BUFFON ASEMA NI VIGUMU JUVENTUS KUTETEA UBINGWA MSIMU HUU

MLINDA mlango, Gianluigi Buffon anaonekana kutishwa na usajili msimu huu, baada ya kusema kwamba itakuwa ni vigumu kwa Juventus kutetea ubingwa wake  wa  Serie A, baada ya mahasimu wao nchini Italia timu za  AC Milan, Roma, Inter  na  Napoli  kusuka vikosi vyake.

Msimu ujao Juventus itakuwa ikisaka kutwaa taji hilo kwa mara ya saba mfululizo, lakini inaonekna itakutana na vikwazo kutoka kwa  timu za  Milan, Roma, Inter  na  Napoli tofauti na misimu iliyopita.

Msimu huu AC Milan inaonekna itakuwa tofauti kuliko  Juventus  kwa kuwa itakuwa na  mastaa kama vile, Leonardo Bonucci na huku ikiwa imewasajili, Lucas Biglia, Andre Silva, Hakan Calhanoglu, Andrea Conti, Ricardo Rodriguez, Mateo Musacchio, Franck Kessie  na Fabio Borini.

Huku pia nyota Rick Karsdorp, Cengiz Under, Aleksandar Kolarov, Maxime Gonalons, Lorenzo Pellegrini  na  Hector Moreno wakiwa wamejiunga na AS  Roma, Inter   wao watakuwa na mastaa kama Borja Valero  na Milan Skriniar, wakati  Napoli wakiwa wamewarejesha nyota kadhaa baada ya msimu uliopita kushika nafasi ya tatu.

Akizungumza juzi mara baada ya mchezo ambao Juve waliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti dhidi ya AS Roma  katika michuano ya Kombe la Mabingwa wa Kimataifa, nahodha huyo alisema:

"Imekuwa ni ziara nzuri na muhimu nchini Marekani kwa ajili ya kujipanga na msimu ujao.”


"Lakini  huu utakuwa ni msimu mgumu kwa  Juventus kwa sababu timu nyingi zimesuka vikosi vyake kama vile, AS Roma, Inter  na  Milan wakati Napoli wamebaki na nyota wake,”aliongeza staa huyo.

No comments