CHOKORAA ALIAMSHA DUDE TWANGA PEPETA, AIFUFUA MAPACHA WATATU


Katika kile kinachoaminika kuwa ni kuibuliwa kwa bifu lingine, mwimbaji wa Twanga Pepeta, Khalid Chokoraa ameirejesha sokoni bendi ya Mapacha Watatu, hatua inayoweza kuleta mtafaruku kati yake na bosi wake Asha Baraka.

Hatua ya Chokoraa pia inaweza ikaleta mtafaruku kati yake na wakurugenzi wenzake wa zamani wa Mapacha Watatu – Jose Mara na Kalala Jr.

Chokoraa ameiambia Saluti5 kuwa Jumapili hii bendi yake itafanya onyesho Magomeni katika ukumbi wa Garden Breeze, lakini pia Jumamosi usiku Mapacha Watatu itakuwa Kigamboni katika ukumbi wa Silver Sharks.

Alipoulizwa ni vipi ataweza kuitumikia bendi yake na ile mwajiri wake – Twanga Pepeta, Chokoraa akasema maonyesho ya Mapacha Watatu yatakuwa katika mfumo wa bonanza yatakayoisha saa 5 za usiku na hivyo  baada ya hapo atawahi kushiriki show za mwajiri wake.

“Maonyesho ya Mapacha yataisha saa 4 au 5 usiku, ndiyo maana sitahangaika na show za Ijumaa na siku zingine, sisi ni Jumamosi na Jumapili tu,” alisema Chokoraa.

Saluti5 ilipomuuliza kama ana baraka za mwajiri wake, Chokoraa akasema anaamini hivyo.

“Niliongea na mama Asha Baraka. Mwanzoni alionyesha kuchukia, lakini baada ya kumwelewesha sana, nahisi mwishoni alinielewa,” anafafanua Chokoraa.

Saluti5 ilijaribu kumpigia Asha Baraka, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Kuhusu haki yaye kutumia jina la Mapacha Watatu wakati alishaachia hisa zake na kurejea Twanga Pepeta, Chokoraa alikuwa na haya ya kusema: “Mapacha Watatu ipo kisheria na itambulikwa kuwa inamilikiwa na watu watatu, Jose Mara, Kalala Jr na Chokoraa.

“Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) walitupa maelekezo kuwa yeyote kati yetu ana haki ya kutumia hilo jina”.

Saluti5 ilipoomuliza Chokoraa kuwa haoni kwamba zitakuja kuibuka bendi tatu za Mapacha Watatu na kuleta mkoroganyo, akasema, hilo sio tatizo, ili mradi tu kila moja ijitofauitishe kwa kuandika Mapacha Watatu chini ya Khalid Chokoraa, chini ya Jose Mara au Kalala Jr.

Chokoraa amesema hana mpango wa kuwatumia wanamuziki wa Twanga Pepeta katika bendi yake hiyo bali atatumia wasanii wa bendi zingine ambapo aliwataja baadhi kuwa ni mpiga solo Super Black, mwimbaji na rapa Frank Kabatano, mpiga drum Martin Kibosho bila kumsahau ‘wa ubavu’ wake Caty Chuma.No comments