CONTE "AWAKATISHA TAMAA" MASHABIKI WA CHELSEA

KOCHA wa Chelsea, Antonio Conte, amesema kwamba itamchukua miaka minne ili kukitengeneza kikosi cha ushindi kitakachoweza kupambana kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Conte ambaye ameshinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita ukiwa msimu wake wa kwanza, lakini anaamini mafanikio yanatengenezwa na msingi imara. 

Na baada ya kukaa msimu mmoja Chelsea, Conte anasisitiza kwamba anahitaji muda zaidi ili kuwa na uhakika wa kutwaa mataji kwenye klabu hiyo.

“Tunahitaji muda,” alisema Conte na kuongeza kwamba inawezekana miaka minne ikatosha kuunda kikosi cha kupambana kunyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakati kocha huyo ana lengo la kukitengeneza kikosi kipya cha Chelsea tayari ameingia katika vita ya maneno na mshambuliaji wake, Diego Costa.

Mshambuliaji huyo kwa sasa yupo Brazil akijifua binafsi huku akikataa kujiunga na Chelsea baada ya kuelezwa na Conte kwamba hayupo kwenye mpango wake.

Licha ya kuwa kocha wa 14 katika klabu ya Chelsea ndani ya miaka 14 tangu Roman Abramovich kuwa mmiliki wa klabu hiyo, kocha huyo anaamini kwamba atapata muda anaohitaji.     

“Hakuna mtu yeyote aliyeninyooshea bunduki kwenye kichwa changu na kuniambia unashinda au unaondoka,”alisema Conte.

“Kuna wakati unaweza kushinda mataji lakini bado haujatengeneza kitu fulani kwa ajili ya maisha yajayo.


Unaweza kushinda na kujiharibia mwenyewe na wakati mwingine hushindi lakini unajiandaa kuwa bora baadaye hivyo tunatakiwa kutengeneza msingi imara lakini kwa sasa hatuna kitu hicho.” aliongeza Muitaliano huyo.

No comments