CONTE AWAPOZA MASHABIKI WA CHELSEA KWA KUWAAMBIA "NITAENDELEA KUINOA CHELSEA"

KOCHA wa Chelsea, Antonio Conte ni kama amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo, baada ya kusema kuwa ataendelea kukinoa kikosi hicho, licha ya kuwapo tetesi kuhusu hatima ya nafasi yake kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu England.

Mapema Julai mwaka huu, Conte alikubali kusaini mkataba mpya wa miaka miwili, baada ya kuiwezesha Chelsea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ukiwa ni msimu wake wa kwanza, lakini amekuwa akiripotiwa kutofurahishwa na jinsi suala la usajili linavyoendeshwa kwenye klabu hiyo ya Stamford Bridge.

Hadi sasa Chelsea imemsajili, Alvaro Morata, baada ya kumkosa Romelu Lukaku, aliyekwenda kujiunga na Manchester United na huku Jose Mourinho akimnasa tena Nemanja Matic na kumpeleka Old Trafford wakati nyota Tiemoue Bakayoko na Antonio Rudiger walikuwa ndio wachezaji pekee waliosajiliwa na Conte.

Hata hivyo, wakati dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa Alhamisi wiki hii, Conte anasema ataendelea kuwatumia wachezaji alionao kwa sasa endapo haitapatikana sura nyingine mpya kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge.

"Mara zote ujumbe wangu kwa mashabiki huwa ni huo huo: Kwa ujumla nitaitumikia klabu na kuimarisha wachezaji na timu yangu," alisema Conte mara baada ya mchezo wao wa juzi ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Everton.

"Mimi ni kocha na wala si meneja na kazi yangu nzuri huwa ipo uwanjani kwa ajili ya kuimarisha wachezaji na timu. Na mara zote wakati unapokuwa unataka kuboresha timu yako ni lazima utoe mawazo yako na baada ya hapo klabu inaweza kwenda sokoni ili kutatua tatizo,” aliongeza Conte.


Alisema kwamba, wakati mwingine inawezekana ama ikashindikana, lakini akasema ni kwamba ni lazima uelekeze nguvu zako uwanjani ili uweze kufanya kazi na wachezaji utakaokuwa nao.

No comments