HAPATOSHI ‘DIMBA MUSIC CONCERT’ MSONDO NGOMA DHIDI YA KOMBAINI YA DANSI


KWA muda mrefu bendi kongwe ya muziki wa dansi Msondo Ngoma imekua kama haina mpinzani jukwaani kiasi cha kujiamini kupita kiasi.

Lakini sasa kumekucha kwani wanamuziki mastaa wa dansi nchini wamejikusanya pamoja ili kuionyesha kazi katika onyesho maalumu linaloitwa DIMBA Music Concertlitakalofanyika Septemba 2 mwaka huu katika Ukumbi Travertine Magomeni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Saluti5 jijini Dar es Salaam meneja wa tukio hilo, Mwani Nyangassa alisema,mastaa hao watachuana na Msondo Ngoma kwa kila upande kuonyeshana umahiri wa kuimba na kulitawala jukwaa.

Aliwataja mastaa hao waliojikusanya pamoja kuikabili Msondo usiku wa siku hiyo kuwa wataongozwa na waimbaji Kikumbi Mwanza Mpango'King Kiki', Hassan Rehani Bitchuka 'Stereo', Hussein Jumbe, Juma Kakere, Karama Regesu, Ally Choky, Nyoshi El Saadat na Muumin Mwinjuma.

Kikosi hicho cha mastaa hao kitakua na wapiga vyombo Saadi Ally 'Machine' kwenye dramu, solo Aldofu Mbinga, rythim Adam Hassan na Hosea Mgohachi atakuwa kwenye bass gitaa.

Aidha, Mwani alisema kinanda kitakua chini ya Juma Jerry wakati tumba zitakung'utwa Salum Chakuku 'Chakuku Tumba' ambapo kwa upande wa ala za upepo watakuwepo Ally Yahaya, Hamis Mnyupe ambao watapuliza trumpet huku Shaabani Lendi akisimama kwenye saksafoni.

"Utakua ni usiku wa mastaa wa dansi kuionyesha kazi Msondo Ngoma kwani miaka ya hivi karibuni imekua ikikosa mbabe katika kila bendi inayoshindanishwa nayo lakini safari hii tumeamua kuwaletea kitu tofauti cha kuleta hamasa ya muziki wetu wa dansi,"alisema Mwani.

Kwa upande wake kkuu wa jukwaa la bendi ya Msondo, Juma Katundu alisema, mastaa hao wajiandae kuangukia pua kwani wao ndiyo baba ya muziki Tanzania.

No comments