KAGERA SUGAR WATAMBA KUFANYA KWELI LIGI KUU MSIMU UJAO

NAHODHA wa Kagera Sugar, George Kavilla ametamba kuwa kikosi chake kina fursa ya kumaliza Ligi Kuu msimu ujao kikiwa nafasi mbili za juu.

LIGI Kuu Tanzania bara ambayo Kagera Sugar ni miongoni mwa timu 16 zitakazoshiriki, itaanza kutimua vumbi Agosti 26, mwaka huu.

Akizungumza jana, Kavilla alisema licha ya ushindani mkubwa unaotarajiwa kuwepo msimu ujao, kikosi chao kimejipanga kufanya vizuri zaidi kutokana na maandalizi ya uhakika wanayofanya kuelekea msimu mpya.

“Kagera imepanga kumaliza msimu ikiwa katika nafasi ya juu zaidi ya ile tuliyomaliza msimu uliopita, msimu ujao tunaitaka nafasi ya pili au ubingwa kabisa, hiyo ndiyo dhamira yetu."

“Najua msimu ujao utakuwa na ushindani mkubwa, lakini hilo si jambo geni kwani linatokea karibu kila msimu, kwa upande wetu tunataka kuandika historia mpya ya Kagera,” alisema Kavilla.

Kagera msimu uliopita ilimaliza Ligi ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Simba iliyokamata nafasi ya pili na Yanga iliyotwaa ubingwa.


Timu hiyo inatarajiwa kufungua pazia la Ligi Kuu Tanzania bara kwa kuivaa Mbao FC kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

No comments