KLOPP ASEMA HANA HAJA YA KUWANIA BEKI MWINGINE WA KATI KIKOSINI KWAKE

KOCHA  wa Liverpool,  Jurgen Klopp amesema kwamba kikosi chake hakina haja ya kuongeza beki mwingine wa kati licha ya kuendelea kuhusishwa kumfukuzia  Virgil van Dijk.

Mwezi Juni  beki huyo wa  Southampton alikuwa akionekana kuwa mbioni kutua  Liverpool  hadi  Reds walipoomba radhi na kuacha kumfukuzia Mholanzi huyo baada ya  Southampton kulalamika kuhusu kuvunjwa sheria za Ligi Kuu kwa jinsi walivyokuwa wakimfukuzia.

Mpaka sasa Liverpool  hawajaongeza nguvu kwenye safu hiyo ya ulinzi wa kati  katika dirisha hili la  usajili, lakini pamoja na kutofanya hivyo Klopp anasisitiza kuwa anajisikia mwenye furaha kwa wachezaji alionao,  Dejan Lovren, Joel Matip, Ragnar Klavan na  Joe Gomez.

Akizungumza mara baada ya mchezo wao wa kirafiki walioibuka na ushindi wa mabao  3-1 dhidi ya  Athletic Bilbao uliopigwa mjini Dublin, Klopp alisema kuwa kwa sasa wana mabeki wa kati wanne na hivyo haoni kama kuna haja ya kuongeza wengine.

"Tuna mabeki wa kati wanne hivyo sidhani kama tunahitaji wengine zaidi,” alisema kocha huyo.

"Kwa sasa nipo vizuri. dirisha la usajili litakuwa wazi hadi Agosti 31 mwaka huu. Hatuwezi kulazimisha kitu  na hatuwezi kupata beki wa kati katika mazingira kama haya,”aliongeza.

No comments