LWANDAMINA "AFUNGA NDOA" NYINGINE NA YANGA SC

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina hana mpango wa kuondoka maana tayari ameongezewa muda wa kuendelea kufanya kazi Jwangwani.

Uongozi wa Yanga umeamua kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja kocha wao George Lwandamina raia wa Zambia baada ya ule wa awali kumalizika Julai 16, mwaka huu.

Katika mkataba wake uliopita, Lwandamina aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kuifikisha katika nusu fainali ya Kombe la FA kabla ya kutolewa na Mbao FC ya Mwanza.

Katibu mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema mchana kuwa wameamua kumuongeza mkataba Lwandamina baada ya kuridhishwa na kazi yake.

“Tunaingia mkataba mwingine wa mwaka mmoja na Lwandamina kwani ule wa mwanzo umeisha na sasa kila kitu kipo tayari hivyo muda wowote tena kwa uwazi kabisa atasaini mkataba mpya.”

“Tumejitahidi kwa uwezo wetu kuboresha mkataba wake mpya kwa kumuongezea maslahi kidogo ili apate motisha ya kufanya kazi yake ipasavyo,” alisema Mkwasa.

No comments