MAJERUHI GEOFREY MWASHIUYA AINGIA GYM KUJITENGENEZEA UHAKIKA WA NAMBA KIKOSINI YANGA

BAADA ya kuumia na kuukosa mchezo wa juzi Jumatano wa Ngao ya Jamii, winga wa Yanga, Geofrey Mwashiuya ameamua kuanza mapema mazoezi ya gym ili kujiweka fiti zaidi aweze kumshawishi kwa haraka kocha wake, George Lwandamina katika kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Mwashiuya ambaye kwa muda mrefu yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha ya kifundo cha mguu, tayari ameanza mazoezi hayo katika gym ya London iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujubu wa daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, Mwashiuya anaendelea vizuri na anafuata ratiba ya mazoezi aliyopewa.

Kwa upande wake, Mwashiuya amesema: “Naendelea vizuri, naamini siku si nyingi nitakuwa fiti kama zamani na kuanza kuitumikia timu yangu."


“Nimepewa program za mazoezi niwe nafanya ili kurudi katika hali yangu ya kawaida na nimekuwa nikifanya hivyo kila siku, nataka niwe fiti kabisa ili kocha Lwandamina aweze kunipa nafasi ya kucheza kwani nafahamu kama nisipokuwa fiti nitaishia kukaa nje tu.”

No comments