MAJERUHI SHOMARI KAPOMBE SASA YUKO FITI

BEKI kisiki wa Simba, Shomari Kapombe amepona na yuko tayari kwa mapambano ya Ligi Kuu ya soka Tanzania bara, imefahamika.

Habari zinasema kwamba beki huyo ambaye aliumia wakati wa mechi ya timu ya taifa ya Tanzania na Rwanda, amepona kabisa baada ya madaktari kumuhudumia kwa kiwango cha juu.

Nyota huyo ambaye amerejea Simba baada ya kuitumikia Azam FC, yeye mwenyewe amekaririwa akisema kwamba hasikii tena maumivu ya nyonga ambayo awali yalikuwa yanamsumbua.

Lakini amesema kwamba sasa amepona kabisa na yupo tayari kuitumikia Simba katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania Barani.

"Kwa sasa naendelea vizuri kwani yale majeraha yangu yamepona na sisikiii maumivu, muda wote naweza kuungana na wenzangu kwa ajili ya mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao,” amesema beki huyo na kuongeza.

“Sifurahii kukaa nje nimekuwa nikipambana kuhakikisha napona haraka na kurejea uwanjani kuipambania timu yangu, kitu cha faraja ni kwamba kwa sasa naweza kufanya hivyo kutokana na kupona kwangu.”

Simba imemsajili tena Kapombe baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Azam na timu ya taifa, lakini bado hajaweza kuitumikia klabu yake hiyo kutokana na maumivu.


Kocha wa Simba, Joseph Omog amekuwa akiwatumia Ali Shomari na wakati mwingine kiraka Erasto nyoni katika nafasi ya ulinzi wa kulia, ingawaje pia beki wote wa Simba ukiachana Jamal Mwambeleko na Mohammed Hussein, wana uwezo wa kucheza nafasi hiyo.

No comments