MAKALA: VIDOMIDOMI HATUKOSI LA KUSEMA KUELEKEA VPL MSIMU WA 2017/2018Na Chiki Mchoma

Msimu wa VPL 2017/2018 u mbioni kuanza na Sisi 'Vidomidomi' lazima tuibuke kusema Machache.

Ndio ee... Lazima tuseme nani wa kutuzuia??...

Wacha tuseme hata kama hutapenda tunachokisema... Sipo Duniani kukuifanya nafsi yako ifurahi bali niko Duniani kuifanya nafsi yangu ifurahi.

Na moja ya furaha yangu ni kupiga Maneno kidogo juu ya hivi Vilabu vyetu Nchini.

Ndio ee... Na nitavisema bila kujali unanuna au unacheka muhimu ni mimi kuongea kwa Weledi zaidi.

Nitavichambua Vilabu Vichache kwa niaba ya Vingine :

AZAM FC:
 Maashaallah... Sasa naiona Azam niliyowahi kuitamani...

Kongole kwako Mtendaji Mkuu Kijana Mchapakazi na Mwenye Maono Makali ABDUL MOHAMED.

Ndio ee... Azam hii haijapata kusikika licha ya kwamba bado haijaanza ligi rasmi lakini mafanikio yao ya Mechi za Kirafiki walizoanzia Nchini Kisha Rwanda na Kumalizia kule Uganda ni Jibu tosha kuwa jina la ABDUL MOHAMED linastahili kuandikwa kwa herufi kubwa.

Maamuzi magumu ya Bodi ya Wakurugenzi yakiongozwa na Mpango Mkakati wa Afisa Mtendaji Mkuu huyu yameleta heshima kubwa sana kwenye kikosi ambacho sasa Makocha wana nguvu Mbele ya Wachezaji na Wachezaji wana Utii Mbele ya Makocha wao.

Hili lilikosekana kwa Muda mrefu sana pale Azam FC.

Timu ilikosa Nidhamu kwa Sauti ya Kocha au hata ya Nahodha John Bocco.

Huwezi kuwa na Wachezaji ambao wanaamini wao ni Muhimu kuliko timu ukadhani utajenga timu... Never!!!

Sasa hata rafiki yangu IDDI ABOUBAKAR anajisikia raha kuendeleza Vijana wapya kwenye Lango la Azam baada ya Kumuibua Aishi Manula mbele ya Aliyekuwa Golikipa namba moja wa Timu hiyo na Timu ya Taifa ya Zanzibar Mwadini Ally.

Kwa sasa Azam FC ni tishio Maradufu kuliko wengi wanavyodhani kuwa imejirudisha nyuma...

Nawahakikishia kwa Azam Hii ni Mpaka Dakika 90 ziishe ndipo ujue kuwa umeifunga Azam FC.

Azam FC hii Naipachika jina la Hapa Kazi Tu Kutokana na Kusheheni Viongozi Makini na Benchi lenye Maamuzi na Zaidi ya Yote kuwa na Kikosi Imara cha Vijana wenye Nia na Uchu wa Kudhihirisha Vipaji na Uwezo wao.
Subirini Mtanambia.


MBEYA CITY:
Japo nimechelewa kidogo ila Namshauri Kaka yangu Emmanuel Kimbe ajitahidi kuijenga tena Mbeya City ya Viwango.

Timu hii kwa miaka hii ya Karibuni imepoteza Morali yake... Imepoteza Mashabiki wake wa Kuililia... Imepoteza Roho ya Paka iliyokuwa nayo wakati inaingia VPL.

Imekuwa rahisi kwenda Sokoine na Kuzoa Point na Kuondoka nazo... Daah..

Kimbe !! Kimbe !! Kimbe !! Sokoine sio Mahala pa Wanyang'anyi kuja kuchukua na kuondoka.

Muda ulipatikana wa kutosha tunategemea kuiona Mbeya City yenye kurudisha nguvu zake na kuamsha Ari ya Mashabiki wake.
Naamini Umenisikia.


SINGIDA UNITED:
Sijui ni kwa Kiasi gani ndugu yangu Mkurugenzi Mtendaji Festo Sanga ameiweka Singida United Mioyoni mwa Wana Singida.

Hilo ni la Muhimu zaidi kabla ya kuchukua point tatu toka timu yoyote pale Jamhuri Dodoma mtakapoanzia Mechi za Awali za Ligi mpaka Mtakaporejea uwanja wa Nyumbani pale Singidani Namfua.

Kiujumla Mkurugenzi Mtendaji umefanikiwa Maeneo kadhaa Makubwa.

1.Kuitangaza Timu yako na Kuipandisha hadhi.

2.Kuwa na Benchi la Ufundi lililo bora Zaidi kwa Sasa Nchini.

3. Kuwa na Kikosi kilichounganika kwa haraka sana.

Haya umefanikiwa sana sana Mana ni Ukweli ulio wazi bila kuvunja heshima ya Vilabu vingine... Singida United mna Benchi la Ufundi bora zaidi kwa Sasa.

Najiuliza vipi kama Mzee Hans angekikamata kikosi cha sasa cha Simba Sports.

Wacha yabaki kuwa Mawazo yangu tu !!


YANGA AFRIKA:
Ni Mashaka matupu kwa Wasiojua Soka...!!

Kuna watu wanadhani Yanga hii ni Dhaifu sana wakiilinganisha na Simba.

Wanachosahau ni kuwa Yanga hii ipo pamoja Muda mrefu kuliko Simba hii inayojiungaunga yenye kikosi kipya kuanzia namba moja hadi kumi na moja.

Mwalimu Mzoefu Lwandamina bado hajawa kipenzi cha Wana Jangwani ila kama akiitumia vizuri nafasi hii aliyonayo sasa nadhani atadhihirisha zaidi ya aliyoyafanya pale Zambia.

Kikosi cha Yanga kiko Vizuri sana japo Mashaka pekee ni hali ya Mtikisiko wa Kiuchumi waliokumbana nao na huo unawatesa mpaka sasa.

Nimependezwa na Mpango kazi wa Katibu Mkuu Mzee 'Charlz Bonny' wa Kuwavuta kundini Wachezaji Wakongwe waliopitia Klabu hiyo ili kuongeza Hamasa kwa Wachezaji.

Niwaambie tu... Falsafa hiyo itafanya kazi kweli kweli kwa kuwafanya Wachezaji wa Yanga kuwa Bora Kisaikolojia kitu ambacho ni muhimu mno kwa Mchezaji yeyote kuwa nacho kuliko pesa.

Ushasahau Maamuzi Magumu ya Yaliyofanywa pale Yanga Mwaka 1996 na Kuzaliwa Kwa 'Yanga Yosso'??... Au umeisahau ile Yanga iliyoenda Kampala kwa Basi na Kurudi kwa Ndege??... We sema ulikuwa hujazaliwa tu ila hawakuwa na Pesa bali walijaa Saikolojia ya Kupambana na hali zao.

Wanaoijua Yanga hawana Hofu... Ila wenye Kuamini katika pesa Tu hawalali kwa Presha.
Tusubiri.

SIMBA SPORTS: :
Hawa wana Matumaini hadi wamepitiliza.

Kila walichokitaka wamekipata... Wanajiamini... Wanaongea.... Wanajidai... Wanaringa...!!!

Ndio ee... Wanastahili kufanya yote hayo kwa kuwa wamejaza majina ya kujidai nayo lakini wamesahau kuwa Kikosi chao ni Kikubwa kuliko Kocha wao !!!

Kocha Omog anapwaya kwenye Kikosi hiki ( Bila kumvunjia heshima ).

Kikosi kimekuwa kipana kiasi anachanganyikiwa nini afanye.

Hata katika Mechi ya Maonesho tu ya Simba Day alijaa presha kiasi Mashabiki wa Baadhi ya Wachezaji kama Said Mohamed 'Nduda' au Jamal Simba Mnyate hawakupata kuwaona Wachezaji wao hasa katika siku hii ya Kihistoria ya Utambulisho wa Wachezaji wa Simba.

Bado hajaweza kumuunganisha John Bocco kuwa Mfungaji huru na Sio kumuacha ateseke kulazimisha kufunga.

Kiufupi Wachezaji Simba wanacheza kwa Uwezo wao zaidi kuliko Muunganiko wa Kiufundi.

Ndio maana nilitamani Kumuona Kocha mwenye 'Levo' ya Hans Van Pluijim kwenye Benchi la Simba kwa aina hii ya Kikosi.

Ngoja ninyamaze mana nasikia anajua Kiswahili siku hizi.


KAGERA SUGAR :
Timu yenye Kocha ninayemkubali sana pembeni ya Mayanga.

Mecky Mexime amekuwa Kocha Mtendaji na Vitendo vyake Viko wazi sana kuliko Maneno.

Hahitaji Wachezaji wenye Majina ila yeye huwapa Wachezaji majina.

Tutaendelea kujifunza kwake mpaka tuchoke.


MTIBWA SUGAR :
Shuleni kuna msemo maarufu wakati wa kuitwa Majina iwapo jana yake hamkuitwa.

Basi ndivyo ilivyo kwa Mtibwa Sugar....

Jana na Leo...

Siku njema Wadau.

Makala hii imeandikwa na Chiki Mchoma
+255 712 885 999.No comments