MARSEILLE WAMMEZEA MATE DIEGO COSTA

WATEMI wa Ligi Kuu Ufaransa maarufu kama League 1, klabu ya Marseille wamesema kwamba wako tayari
kufungua bahasha kwa ajili ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa Chelsea, Diego Costa.

Marseille wamesema kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yao kwamba wanataka kumsajili Diego Costa wakiamini kwamba straika huyo atakuwa na furaha kwenye kikosi chao.

Costa ambaye alifukuzwa na meseji ya kocha wa Chelsea, Antonio Conte amedai pia kwamba juzi ametumiwa meseji nyingine na kocha huyo raia wa Italia.

Lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, bado yuko nyumbani kwao alikozaliwa Brazil, akisubiri kujua namna gani anaweza kuondoka kwenye kipindi hiki cha uhamisho wa wachezaji. 

Lakini pia klabu yake ya zamani ya Atletico Madrid imesema kwamba iko katika mipango ya kumrejesha nyota huyo japo kwa mkopo.

Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amesema kwamba anaweza kuwa katika wakati mzuri wa kumsajili nyota huyo ingawa anajua kwanba klabu yake imezuiwa kufanya usajili hadi mwezi Januari mwakani.

Hata hivyo, Madrid wanaweza kuruhusiwa kufanya usajili kama usajili huo utakuwa wa kupata mchezaji kwa mkopo na Chelsea hawaonekani kutaka kumwachia Diego kwa njia hiyo bali kwa mauzo.

Lakini hayo yakiendelea rais wa klabu hiyo ya Ufaransa Jacques Henri Eyraud amesema kwamba anaweza kujisikia mwenye amani zaidi ikiwa atapata saini ya mchezaji huyo.

“Napenda sana namna anavyocheza, ni mmoja wa nyota ambao nikiwapata katika klabu yangu nitalala usingizi,” amesema rais huyo.


“Yuko katika wakati mgumu kwa sasa na hana amani, najua kwamba akija huku anaweza kuwa katika amani na furaha wakati wote,” amesema.

No comments