MASTAA WA DANSI WAIKAMIA MSONDO NGOMA KWENYE DIMBA MUSIC CONCERT SEPTEMBA 2


MAGWIJI wa muziki wa dansi waliounda kikosi cha timu ya Taifa ya muziki huo kuikabili Msondo Ngoma wameapa kula sahani moja na bendi hiyo usiku wa DIMBA Music Concert utakaofanyika Septemba 2 mwaka huu katika Ukumbi wa Traventine Magomeni jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na Saluti5 kwa niaba ya wenzao,waimbaji Juma Kakere,Hussein Jumbe na Mwinjuma Muumin walisema Msondo Ngoma wajiandae kupata aibu kwa namna walivyojiandaa kuwaonyesha ubora walionao katika uimbaji na kulitawala jukwaa.

Kakere alisema,onyesho hilo linakwenda kumaliza zama za ufalme wa Msondo baada ya kutamba kwa muda mrefu ambapo mashabiki watakaofika siku hiyo watakutana na 'suprise' kibao kutoka kwa mastaa.

Kwa upande wake Jumbe alisema anaijua Msondo kinagaubaga hivyo tayari wanazo silaha za kuiangamiza mapema kwani hawatarajii kama watasogea hata raundi ya tatu ya usiku hiyo.

"Nimefanya kazi na Msondo Ngoma nawajua vyema,hawanisumbui kwani wengi ya wanamuziki wao ni vijana wangu nawajua namna ya kuwapoteza jukwaani ili kudhihirisha ubora wa sisi mastaa wa muziki wa dansi,"alisema, Jumbe.

Kwa upande wake Mwinjuma Muumin,alisema,siku hiyo usiku wa siku hiyo patachimbika kwani yeye binafsi atawashangaza Msondo na nyimbo mpya na zile zamani alizoziandaa.

Mbali ya Jumbe,Kakere na Muumin kikosi cha mastaa hao wa muziki watakaopambana na Msondo kinaundwa na waimbaji Kikumbi Mwanza Mpango' King Kiki',Hassan Rehani Bitchuka 'Stereo', Karama Regesu na Ally Choky.

Kwa upande wa vyombo watakuwepo wapiga vyombo Saadi Ally 'Machine' kwenye dramu,gitaa la solo likitekenywa na Aldofu Mbinga wakati besi litangurumishwa naHosea Mgohachi.

Aidha,kinanda,kitatekenywa Juma Jerry wakati tumba zitakung'utwa Salum Chakuku 'Kuku Tumba'ambapo ala za upepo watakuwepo Ally Yahaya, Hamis Mnyupe Tarumbeta na Shaabani Lendi kwenye Saksafoni.

"Utakua ni usiku wa mastaa wa dansi kuionyesha kazi Msondo Ngoma kwani miaka ya hivi karibuni imekua ikikosa mbabe katika kila bendi inayoshindanishwa nayo lakini safari hii tumeamua tuwaonyeshe kazi, "alisema.


No comments