MTIBWA SUGAR YAPANIA KUONYESHA MAAJABU MSIMU HUU

WAKATI wa Ligi Kuu ya VodaCom Tanzania bara msimu wa 2017/18 umeanza juzi Jumamosi, klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imepania kufanya vizuri chini ya kocha wake, Zuberi Katwila.

Beki mahiri wa klabu hiyo, Salum Kanoni Kupela aliyesajiliwa kutoka Mwadui FC ya Shinyanga, ameongea juu ya matarajio yake msimu ujao.

“Nadhani kitakachotubeba ni ushirikiano na kujituma kwa kufuata maelekezo ya kocha wetu ninayemuona anapigania timu, hivyo nadhani msimu huu tutafanya vizuri zaidi na kushika nafasi za juu, wachezaji waliosajiliwa na waliokuwepo nao wana uwezo mkubwa sana, kikubwa Allah atuongoze,” alisema Kanoni.

Beki huyo wa zamani wa Simba SC na Kagera Sugar amesifu maandalizi yao ya msimu huu kwamba yamekuwa mazuri.

“Benchi la ufundi limekuwa likitupa mazoezi na maelekezo bora kabisa, pia tumekuwa tukijengwa kasaikolojia, hakika msimu unaoanza nawakaribisha mashabiki wa Mtibwa Sugar kuhudhuria kwa wingi uwanjani watupe ushirikiano wao, nina imani kwa pamoja kuwepo kwao ni faraja kubwa kwetu," aliongeza Kanoni.

Kanoni amesema michezo ya kirafiki waliyocheza imewasaidia kujuana na kurekebisha makosa yaliyojitokeza.


“Tumepata michezo mingi ya kirafiki na ilikuwa kipimo tosha kwetu na michezo hii imetusaidia kutengeneza muunganiko kwa kuwa tupo wachezaji wageni na wa zamani, hivyo ili tuzoeane vizuri ilibidi tucheze michezo mingi, nadhani hadi sasa tumeelewana na tuko tayari kwa msimu mpya,” aliongeza mchezaji huyo.

No comments