MUUMIN ‘AITEKA’ MWANZA VILLA PARK …Double M Plus yapokewa kwa kishindo


Mwimbaji Mwinjuma Muumin amepokewa kwa kishindo jijini Mwanza ambapo yeye na bendi yake ya Double M Sound walifanya show bab kubwa ndani ya Villa Park wikiendi iliyopita.

Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zikawa ni siku tatu mfululizo za burudani bila kikomo ambazo zilidhihirisha kuwa Kocha wa Dunia bado yuko njema mikoani licha ya muziki wa dansi kukumbwa na ‘baa la njaa’.

Akiongea na Saluti5 baada ya maonyesho hayo ya siku tatu, Muumin akasema show hizo zimefungua njia kwake ambapo amepokea simu za mialiko kutoka miji ya Bukoba, Musoma, Kahama na Geita.

Aidha, Muumin amesema wiki hii pia atakuwa jijini Mwanza hapo hapo Villa Park kuziba nafasi ya bendi ya nyumbani Super Kamanyola ambayo imesimamisha maonyesho yake kwa wiki mbili.

Alipoulizwa ni kwanini aliondoka kimya kimya kwenda ziara hiyo ya Mwanza bila fujo za matangazo, Muumin akasema hali ya muziki wa dansi imekuwa ngumu sana, kuna mambo mengine bora uyafanye kimya kimya tu.

“Siku hizi muziki wa dansi hata kwenda mikoani imekuwa sawa na kwenda Muscat, unaweza ukakutana na figisu figisu nyingi kutoka kwa wapinzani wako, watu wakakukatizia denge tenda ikayeyuka,” alisema Muumin huku akicheka.

No comments