"NEYMAR ANAWEZA KUJA KUWA MCHEZAJI BORA ZAIDI DUNIANI" ATABIRI KOCHA WA PSG

KOCHA wa timu ya  Paris Saint  Germain, Unai Emery, ni kama amemtabiria makubwa nyota wake  mpya, Neymar, baada ya kusema kuwa kulingana na kiwango cha staa huyo anaweza kuwa mchezaji bora zaidi wa dunia.

Fowadi huyo wa Kibrazil ameizoea haraka   timu yake hiyo mpya aliyotua katika dirisha la usajili wa majira haya ya kiangazi kwa kitita kilichoweka rekodi ya dunia cha pauni mil 198 kutoka Barcelona.

Neymar alianza kufungua kitabu cha mabao katika mchezo wake wa kwanza tu wa Ligue 1 wikiendi iliyopita kwa kufunga bao moja, huku akimtengenezea mwenzake, Edinson Cavani, bao moja na kuisaidia timu yake kuinyuka Guingamp mabao 3-0.

Kwa kiwango hicho, Emery anaamini Neymar atazidi kuimarika ndani ya timu hiyo na hata kuweza kushinda tuzo ya Ballon d'Or sambamba na kuisaidia PSG kutwaa mataji mbalimbali makubwa.

“Neymar ni mchezaji mzuri, mmoja wa walio bora duniani,” alisema Emery.

“Lakini kiubinadamu, ni mtu mmoja safi hata akiwa na wenzake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na akiwa dimbani.

“Wengine waliopo hapa ni wachezaji wazuri na wana furaha kuona mchezaji kama Neymar yupo PSG. Ndicho nilichokitaka,” alisema.

“Tunataka kufika mbali zaidi tukiwa naye hapa na kumsaidia awe mchezaji bora zaidi. Tutajituma zaidi kumboresha na yeye atajituma kwa manufaa ya klabu. Kwa pamoja tutakuwa bora kama timu,” aliongeza.


Kiwango cha Neymar dhidi ya Guingamp kiliwavutia wengi, lakini Emery alivutiwa zaidi na jinsi staa huyo alivyokuwa akisaidia hata katika sekta ya ulinzi.

No comments