NIYONZIMA ASEMA ANAFURAHIA MAISHA NDANI YA SIMBA SC

KAMA ulikuwa unadhani kwamba kilichomfanya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima kutua Simba ni pesa, hesabu zako zitakuwa hazijakaa sawa.

Kiungo huyo amefichua kile ambacho kimemfanya aikache Yanga na kutua Simba kuwa sio pesa, badala yake akasema ni mahaba na amani.

Haruna amekuwa nyota mkubwa kwa sasa katika Simba na wapenzi wa klabu hiyo hupagawa wanapowaona wakicheza kwa pamoja na Mganda Emmanuel Okwi, wachezaji ambao wanatajwa kuwa ghali zaidi kwa sasa.

Niyonzima amesema kuwa mbali na soka yeye pia ana kipaji cha juu cha uimbaji lakini amechagua soka kuwa sehemu kubwa ya maisha yake.

Akihojiwa Haruna amesema kwamba anafurahia maisha ndani ya Simba lakini kikubwa zaidi anafurahi kuwepo Tanzania.

Amesema kwamba Tanzania ni nchi yenye amani kubwa na hivyo kuendelea kubaki hapa nchini huku akiwa Simba anajihisi mwenye amani wakati wote.

“Kama ukiwa na fedha nyingi halafu huna amani ni sawa na bure,” amesema Haruna katika mahojiano hayo.

“Mimi ni muimbaji, naweza kuingia studio na kuimba kabisa, lakini watu wengi hawajui hilo,”alisema Niyonzima kuonyesha kwamba ana vipaji vingi.


Kuhusu uwepo wake Tanzania, Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda alisema: “Chochote ninachokifanya nahisi nipo nyumbani, nikiwa Tanzania nimepata watoto, sijawahi kukaa nchi nyingine muda mrefu tangu nilivyoanza soka kama ilivyo hapa, hivyo nina amani kubwa kuwepo Tanzania.”

No comments