NIYONZIMA: NJOONI MUONE "MUZIKI" WANGU AGOSTI 23 UWANJA WA TAIFA

KIUNGO mpya wa Simba, Haruna Niyonzima amewaita mashabiki wa timu yake kufika kwa wingi katika mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, itakayochezwa Agosti 23, mwaka huu, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Niyonzima alisema kuwa mashabiki wa Simba wanatakiwa kwenda kushuhudia atakavyofanya mambo yake.

Niyonzima alisema anaamini siku hiyo akiamka vizuri basi mashabiki wa Simba watafurahia ujio wake ndani ya timu hiyo.

Alisema kama ilivyo ada timu hizo zinapokutana kunakuwepo na ushindani mkubwa bila kuangalia udhahifu wa timu yoyote kati yao.

Niyonzima alisema anatarajia kukabiliana na changamoto katika mechi hiyo na amejipanga kuhakikisha anaisaidia timu yake mpya kuibuka na ushindi.

“Ni mchezo mgumu lakini siwezi kuuzungumzia sana isipokuwa ujue siwezi kucheza pekee yangu bali nitajaribu kutoa kile nilichonacho kwa kushirikiana na wenzangu Mwenyezi Mungu akinisaidia nikaamka vizuri nadhani nitafanya kitu kizuri,” alisema Niyonzima.

“Nawaahidi mashabiki wa Simba kuwalipa fadhila kutokana na kunipa heshima ya kipekee kwa kukubali uwezo wangu,” alisema Niyonzima.


Niyonzima amesajiliwa na Simba katika dirisha kubwa la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mkataba wa miaka miwili akitokea kwa mahasimu wao, Yanga.

No comments