PAPII KABAMBA KUTIBU MAPUNGUFU YA ULINZI YANGA

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina amegundua mapungufu makubwa katika safu yake ya ulinzi na haraka amewaambia mabosi wa timu hiyo wamshushe kiungo Papii Kabamba ambaye anawasili muda wowote tayari kwa kazi ya kusuka safu hiyo.

Lwandamina amegundua kwamba mabeki wake hao wanatakiwa kwanza kupata uimara kutoka katika safu ya kiungo mkabaji ambayo anaamini pakitulia hapo atapata muafaka wa nani acheze katika ulinzi.

Katika mchezo wa Jumamosi ambao walikosekana Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Lwandamina alitaka kuwaangalia Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vicent ‘Dante’ ambapo katika kambi yao ya maandalizi ya Unguja Zanzibar anataka kuwaunganisha Yondani na Ninja ambaye atafanyiwa msasa mkubwa.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Kabamba ambaye alikuwa awasili juzi lakini tiketi yake ilikuwa na makosa madogo, sasa anatarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.

Akishawasili Kabamba moja kwa moja atasafirishwa mpaka Unguja ili kuungana na kikosi kizima kilichoondoka jana asubuhi kwa kambi fupi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba Agosti 23.


Hata hivyo Lwandamina anaweza kupata unafuu mkubwa endapo Kabamba atawasili kutokana na kiungo huyo pia anaweza kucheza kama beki wa kati kama alivyofanya katika kikosi chake cha zamani cha Mbabane Swallows.

No comments