PETIT MAUZO: ANAYESEMA CHRISTIAN BELLA ANA ROHO MBAYA AJIANGALIE MARA MBILI


Mwimbaji tegemeo wa Malaika Band, Petit Mauzo (pichani), amemimina sifa kwa bosi wake Christian Bella na kumtaja kama mmoja kati ya watu wema kabisa aliowahi kukutana nao.

Petit Mauzo ambaye ni mmoja wa wasanii waanzilishi wa Malaika Band, akasema Bella ni mtu anayethamini kazi na hivyo humpenda sana msanii anayethamini kazi.

Akiongea na Saluti5, Petit alisema: “Nimekaa na Bella kwa muda mrefu, sijawahi kukwaruzana nae, naheshimu mipaka yangu na yeye anaheshimu wajibu wake kwangu. Ni mtu mwema sana.

“Kama kuna mtu anasema Bella ana roho mbaya basi ajiangalie mara mbili, pengine ni yeye ndiye mwenye tatizo.

“Wako wasanii wasio na shukrani, wasiothamini watu waliowatoa kimuziki na badala yake wanaingiza dharau na ushindani dhidi ya watu hao waliowasaidia, lakini mwisho wa siku wanapotea kwenye game”.

“Mimi nasema wazi, Bella ndiye aliyenitoa kimuziki hapa Tanzania, najua amenizidi kwa kila kitu kuanzia kimuziki hadi kimaisha, najifunza mambo mengi kutoka kwake, siwezi kumdharau hata siku moja.”

No comments