RAIS WA MICHUANO YA LIGI KUU HISPANIA AMPONDA NEYMAR

RAIS wa michuano ya Ligi Kuu Hispania, La Liga, Javier Tebas amemponda straika wa Barcelona, Neymar akisema kwamba wangeweza kupata pigo kubwa kwenye soka lao endapo mastaa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wangeondoka na wala sio kwa huyo anayewindwa na Paris Saint-Germain.

Kwa sasa PSG wanaripotiwa kufikia dau la Euro milioni 222 linalotakiwa kuvunja mkataba wa  Neymar katika klabu ya  Barcelona, lakini  Tebas anasema kuwa  kuvunja rekodi ya usajili kwa kutoa kiasi kama hicho pia kunaweza kusababisha kukiuka kanuni za kimataifa zinazohusu matumizi ya fedha.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Neymar alicheza pamoja na Messi dhidi ya  Ronaldo katika mchezo ambao Real  Madrid walinyukwa  3-2 katika michuano ya Mabingwa wa Kiamataifa uliofanyika mjini Miami na  Tebas anasema kuwa haoni kama ni shida endapo staa huyo mwenye umri wa miaka 25 anayekipiga pia kwenye timu ya Taifa ya  Brazil akiondoka Camp Nou.

"LaLiga  na  Barcelona ni kubwa kuliko Neymar," alisema Tebas  katika mahojiano la jarida la  Mundo Deportivo.

"Ningeingiwa hofu endapo kama  Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wangekuwa wanaondoka,”aliongeza rais huyo.

Tebas alikwenda mbali zaidi akisema kuwa wataishitaki PSG endapo itaamua kuvunja kanuni za  FFP bila kujali aidha kama Neymar atashawishiwa kwa kiasi hicho kwenda kujiunga na vinara hao wa  Ligue 1 kwa kile alichodai haiwezekani wakatoa fedha kubwa ambayo inazidi matumizi ya klabu kubwa kama Barcelona ama Real Madrid.

No comments