REFA WA KISOMALI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI

MWAMUZI  maarufu katika mchezo wa kandanda nchini Somalia amepigwa risasi na kuuawa karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu.

Osman Jama Dirah, ambaye alisimamia mechi za kanda na kimataifa, aliuawa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati  akiondoka msikitini kurejea kwake nyumbani katika mtaa wa Wardhigley.

Taarifa zinasema wanaume wawili waliokuwa na bastola walimfatulia risasi mara kadhaa.

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Somalia Anas Ali Mohamud amenukuliwa akisema aliwaona wauaji wakiondoka eneo la mauaji.

Alisema maofisa wa usalama walifika eneo hilo baadaye lakini hadi kufikia sasa hawajafanikiwa kuwakamata wahusika.

Mwandishi wa BBC , Ahmed Adan alisema kuuawa kwa Osman Jama Dirah ni pigo kubwa sio tu kwa tasnia ya soka nchini Somalia bali kwa sekta yote ya michezo nchini humo.

Alikuwa miongoni mwa marefa maarufu zaidi nchini humo tangu kusambaratika kwa serikali kuu miaka 27 iliyopita.


Dirah alifahamika kama mwamuzi bora zaidi na alihudumu katika kamati ya waamuzi katika Shirikisho la Soka la Somalia.

No comments