SAID NDEMLA KUTIMKIA SWEDEN WAKATI WOWOTE

SASA ni dhahiri kwamba kiungo mtundu uwanjani wa Simba, Said Ndemla mambo yake yameiva na wakati wowote anaweza kuondoka na kwenda Ulaya.

Habari zinasema kwamba Ndemla alikuwa aondoke tangu Jumamosi iliyopita lakini kambi ya maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamiii dhidi ya Yanga ndio ambayo imemchelewesha.

Lakini sasa taarifa zinasema kwamba nyota huyo anatarajiwa kuondoka nchini muda wowote kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Sweden.

Ndemla anatarajiwa kwenda kucheza katika timu ambayo anacheza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu ya Athletic Football Club ya nchini humo.

“Kila kitu kinakwenda sawa,tulikuwa tunasubiri mechi hii ya Yanga imalizike, tunashukuru kwamba imekwisha salama na sasa Ndemla anaweza kuondoka wakati wowote,” amesema mtu mmoja wa karibu na kiungo huyo.

Ndemla anakwenda kufanya majaribio kwenye klabu hiyo na kama dili hilo litakwenda sawa, nyota huyo anaweza kujiunga moja kwa moja.

Iwapo Ndemla akifuzu katika majaribio hayo na kuuzwa kwenye klabu hiyo, atakuwa ni mchezaji wa pili kuondoka katika klabu ya Simba kwa sasa baada ya hivi karibuni beki wa timu hiyo, Abdi Banda kutimkia Afrika Kusini kwenye klabu ya Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.


Hata hivyo, tofauti na alivyoondoka Banda ambaye alikuwa amemaliza mkataba, Ndemla anauzwa moja kwa moja na Simba watakuwa wamenufaika na mauzo ya kiungo huyo mwenye mashuti makali uwanjani.

No comments