SIFA POLITAN WAENDELEA KUJIWEKA SAWA NA MSIMU MPYA WA LIGI DARAJA LA PILI

WACHEZAJI wa Sifa Politan wameendelea kujifua katika ufukwe wa bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya wa daraja la pili taifa.

Timu hiyo ilifanikiwa kufuzu hatua hiyo baada ya kufuzu katika kituo cha Lindi Ligi ya Mabingwa wa mkoa msimu uliopita.

Akiongea jana, Ofisa Habari wa Sifa Politan, Garibu Mgomi alisema wachezaji wao wanaendelea kufanya mazoezi ili waweze kuwa fiti kabla ya kuanza kwa Ligi hiyo.

Mgomi alisema malengo yao ni kutaka kufanya vizuri kwenye Ligi hiyo ili waweze kupanda daraja la kwanza Tanzania bara.

“Kwa kweli wachezaji wapya tuliowasajili wameonyesha kiwango cha juu cha uchezaji, tuna imani watafanya vizuri msimu ujao,” alisema Mgomi.


Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo ni Khalid Gede, Twaha Magoha, Jafari Gonga, Abdul Hassan na Abdallah Mbilu.

No comments