SIMBA "MWENDA POLE" AWATIA HOFU MASHABIKI WAKE KUELEKEA MTANANGE WA NGAO YA HISANI KESHO

MWENENDO wa kikosi cha timu ya Simba kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya mahasimu wao Yanga umeanza kuwatia hufu mashabiki wa klabu hiyo kutokana na matokeo waliyopata katika mechi za kirafiki walizocheza mpaka hivi sasa.

Katika mechi zake tano za kirafiki ambazo wamecheza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefanikiwa kufunga jumla ya mabao matatu tu huku pia ikiwa imeruhusu mabao mawili katika wavu wake.

Mashabiki wa Simba waliokuwepo kwenye mechi dhidi ya Mlandege iliyochezwa kwenye uwanja wa Aman walisikika wakilaumu safu ya ushambuliaji baada ya kuonyesha kuwango duni kwenye mechi hiyo lakini pia wamekuwa wakituma maoni kupitia mitandao ya kijamii wakionyesha hali ya hofu.

“Huu ndio mtindo wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa bila kuangalia kama wameisha au la unaweza kuja kutugharimu siku moja, ona namna tunavyoangaika kupata matokeo dhidi ya timu ndogo,”alisema Juma Mbonde shabiki aliyekuwepo uwanjani.

“Tuna kikosi kizuri chenye mchanganyiko wa wachezaji wazoefu lakini mechi za Simba na Yanga huwa hazielewi lolote linaweza kutokea, unaigiza timu uwanjani kwa kujiamini mwisho wa siku unaondoka kichwa chini,” alimaliza.

Simba na Yanga zinainaingia uwanjani kesho katika mchezo wa kuwania Ngao ya Hisani ambapo timu hizo zimeweka kambi visiwani Zanzibar kwa ajili ya kufanya maandalizi kama ilivyo kawaida yao.


Katika mchezo huo wa kesho, Simba inaingia uwanjani ikiwa na hali ya kujiamini kuliko Yanga na hii ni kutokana na aina ya usajili ambao wamefanya ambapo hata hivyo safu yake ya ushambuliaji bado haijaonyesha makali, hali iliyoanza kuleta hofu.

No comments