SIMBA YATAKIWA KUREJESHA NGAO YA HISANI


Kutokana na uzembe uliotokea, Chama cha Soka nchini (TFF) kimeitaka klabu ya Simba irejeshe Ngao ya Hisani iliyotwaa jana baada ya kuichapa Yanga 5-4 kwa mikwaju ya penalti.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya 0-0 katika muda wa kawaida na kulazimika mshindi kupatikana kwa njia ya matuta.

Hata hivyo, Simba imetakiwa irejeshe Ngao hiyo ya Hisani ili ikafanyiwe marekebisho yaliyotokana na makosa ya kiuandishi ambapo iliandikwa SHEILD badala ya SHIELD, hali iliyopelekea malalamiko mengi kutoka kwa wapenda soko kupitia mitandao ya kijamii.

Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka TFF inasema:
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linaomba radhi wanafamilia wote wa mpira wa miguu kutokana na makosa ya maandishi yaliyoonekana kwenye utambulisho wa Ngao ya Jamii iliyotolewa Jumatano Agosti 23, 2017.

Ngao hiyo ilitolewa mara baada ya mchezo uliokutanisha timu za Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini. Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Yanga na kutwaa Ngao hiyo.

Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu popote pale, TFF hatujapokea vizuri mwonekano wenye makosa kwenye Ngao hiyo ya Jamii kama ambavyo wadau hawajapokea vema suala hili.

Kutokana na makosa hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, tayari amechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika kadhalika kuwasiliana na uongozi wa Simba SC kuirejesha Ngao hiyo ili kufanyiwa marekebisho yatakayobaki kwenye kumbukumbu sahihi.

Hatutegemei tukio kama hili kujirudia tena.


No comments