TWANGA PEPETA MBIONI KUACHANA NA CHOKORAA …sasa kuna bendi mbili za Mapacha


Bendi ya The African Stars “Twanga Pepeta” inakaribia kuachana na mwimbaji wake Khalid Chokoraa ambaye ameanzisha upya bendi ya Mapacha Watatu.

Wakati Chokoraa akiiambia Saluti5 Jumamosi mchana kuwa Mapacha Watatu ni mradi wake wa pembeni na kwamba ana ruhusa kutoka kwa bosi wake Asha Baraka, sasa imebainika kuwa hakuomba idhini na wala hakuruhisiwa kuanzisha bendi nyingine huku akiwa bado ni mtumishi wa Twanga Pepeta.

Akiongea na Saluti5, mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema Chokoraa hakuruhusiwa kutumikia bendi mbili kwa wakati mmoja.

Asha Baraka anasema: “Ijumaa usiku niliona tambara la tangazo la bendi yake pale Magomeni Garden Breeze, nikashangaa, sikuwa najua hicho kitu.
“Nilipofika Bulyaga Bar kwenye show ya Twanga usiku huo huo wa Ijumaa, nikamwita Chokoraa na kumuuliza kulikoni hadi anatuletea ‘fujo’ kwenye biashara, nikamwambia hii haikubaliki na ikibidi ni bora aondoke atuachie bendi yetu.

“Hakuwa na la maana la kusema zaidi ya kuniambia mama nitakutafuta tuongee vizuri.”

Mapacha Watatu chini ya Khalid Chokoraa ilianza maonyesho yake Jumamosi huko Kigamboni katika ukumbi wa Silver Sharks  na kufuatiwa na show ya Jumapili Magomeni Garden Breeze.

Hii maana yake ni kwamba sasa kuna bendi mbili za Mapacha – Mapacha Music Band ya Jose Mara na Mapacha Watatu ya Chokoraa.

Asha Baraka ameiambia Saluti5 kuwa Chokoraa hakuwa na mkataba wa moja kwa moja na Twanga Pepeta bali alikuwa na makubaliano na wadau wa bendi ambao wao ndiyo walioingia gharama ya kumrejesha kundini ikiwa ni pamoja na kumnunulia gari.

“Sikuwa na mpango wa kumchukua Chokoraa lakini wadau wa bendi ndiyo walioamua hilo na walikubaliana aitumikie Twanga kwa miaka miwili,” alisema Asha Baraka ambaye alifafanua kuwa jukumu la Twanga ilikuwa ni mshahara tu.

Asha Baraka amesema Chokoraa bado ana nafasi ya kusitisha bendi yake ya Mapacha Watatu na kumalizia mkataba wake wa kuitumikia Twanga kama alivyokubaliana na wadau wetu wakati anachukua pesa, au arejeshe pesa za watu na aendelee na bendi yake.

Mkurungezi huyo wa Twanga akasema ni vema sasa wadau wanaotaka kuisaidia bendi wafanye hivyo moja kwa moja kwa menejimenti badala ya wao kumalizana na wasanii, hatua ambayo huleta sintofahamu mbele ya safari.

Chokoraa alirejea Twanga Pepeta mwezi April mwaka jana na hadi sasa bado hajafanikiwa kuachia hewani hata wimbo mmoja kupitia Twanga.

No comments