VUMBI LA LIGI KUU KUZITIMUA NYASI ZA VIWANJA SABA JUMAMOSI HII

UTAMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaanza wikiendi hii baada ya juzi jumatano kufunguliwa rasmi kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba mchezo uliopigwa uwanja wa wa taifa jijini Dar es Salaam.

Viwanja saba vitatimua vumbi wikiendi hii huku kila timu ikiziweka hadharani silaha zake baada ya kufanya usajili wa nguvu na kutaka kuhakikisha inaibuka na pointi tatu kwenye mchezo wake wa kwanza.

Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, watashuka dimbani Jumapili kwenye uwanja wa taifa kuwakaribisha Lipuli kutoka Iringa ambao wamepanda daraja msimu huu.

Mechi za Jumamosi hii zitashuhudia Simba ikiwa kwenye uwanja wa taifa kucheza na Ruvu Shooting kutoka Pwani, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa baina yao.

Azam FC wao watakuwa ugenini mkoani Mtwara kwenye uwanja wa Nangwanda kucheza na Ndanda ambayo msimu uliopiota ilipanda Ligi Kuu na ambayo inaonekana kuwa na kikosi bora.

Singida United ambayo imepanda daraja msimu huu ikiwa pia imefanya usajili mkubwa wa wachezaji wengi wa kigeni, itaanza kampeni yake mkoani Shinyanga wakati itakapokuwa ugenini kucheza na Mwadui FC.

Vijana hao wa Singida wananolewa na kocha wa zamani wa Yanga Mholanzi Van Pluijim.

Kwa upande wao Mtibwa Sugar watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Manungu pale Turiani kucheza Stand United, huku ndugu zao Kagera Sugar waliopo chini ya kocha Mecky Mexime watakuwa kwenye uwanja wao wa Kaitaba mkoani Kagera kucheza na Mbao FC ya Mwanza ambayo ilipanda daraja msimu uliopita.

Wageni kwenye Ligi hiyo, Njombe Mji ambayo ilipanda daraja msimu huu itakuwa nyumbani kucheza na majirani zao Prison ya Mbeya kwenye uwanja wa Sabasaba.


Mechi ya mwisho kwa Jumamosi itakuwa ni kati ya Mbeya City dhidi ya Majimaji ya Songea, mchezo utakaopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

No comments