WACHEZAJI SIMBA WASEMA OMOG ANAWAKOMOA KATIKA MAZOEZI

KOCHA wa Simba Joseph Omog amekuwa akiwapa mazoezi magumu wachezaji wake ambao sasa wanakiri kwmba kocha huyo hataki mzaha.

Baadhi ya wachezaji walioko katika kambi ya Simba wamesema kwamba mazoezi ambayo Omog na wasaidizi wake Jackson Mayanja na Muharami Mohammed anayewanoa makipa ni hatari.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi kutwa mara tatu, wakati mwingine mpaka unaona kwamba kocha anataka nini kwetu? Lakini ni kutuweka sawa kwa ajili ya Ligi” amesema mmoja wa wachezaji wa Simba.

Mchezaji huyo amesema kwamba hata walipokuwa kambini Afrika Kusini kocha huyo hakuwahi kuwapa mazoezi magumu kama anayowapa sasa.

“Tunafanya mazoezi magumu sana, na kusema kweli mchezaji kama ni mvivu huwezi kuyaweza mazoezi haya,” amesema mchezaji huyo na kuongeza.


Katika mazoezi hayo, kipa Said Mohammed “Ndunda” ameumia goti na kushindwa kumaliza mazoezi na wenzake juzi jioni kwenye uwanja wa ngome uliopo Fuoni.

Hata hivyo Ndunda mwenyewe amesema kwamba inawezekana amepata mshtuko wa kawaida tu.

“Nimeshtuka goti wakati wa mazoezi na nasikia maumivu, lakini daktari ameniambia kuwa sio tatizo kubwa sana na litapona muda si mrefu”, alisema kipa huyo.

Kama hali ya kipa huyo haitatengamaa, ni wazi kuwa nafasi yake itazibwa na kipa namba tatu, Emmanuel Mseja  alisajiliwa kutoka Mbao FC.


Mbali na Ndunda pia majeruhi wengine katika kikosi hicho ni beki Shomari Kapombe na mshambuliaji  John Bocco ambao hata hivyo taarifa zinasema wanaendelea vizuri sana.

No comments