WALLENCE KARIA AAHIDI KURUDISHA HADHI YA SOKA LA BONGO

RAIS mpya wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Wallence Karia amesema kuwa mchezo wa soka unapendwa na watu wengi lakini kutokana na ubadhifu wadhamini wanakimbia hivyo lengo lake kuu ni kuhakikisha anarudisha hadhi ya mchezo huo.

Karia alifanikiwa kuibuka kidedea kwenye kiti cha urais baada ya kupata kura 95 sawa na asilimia 74.22 ambazo hazikuweza kufikiwa na wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.

Karia ameibuka mshindi katika nafasi ya urais baada ya kuwashinda wapinzani wake Ally Mayay na Shija Richard ambao wote walipata kura tisa huku Iman Madega akipata kura nane, Fredrick Mwakalebela kura tatu na Emmanuel Kimbe aliyepata kura moja.

“Nahitaji kurejesha hadhi ya soka hapa nchini kwa kutengeneza mazingira bora yatakayowavutia wachezaji,” alisema kiongozi huyo.

Baada ya kuapishwa kuwa rais mpya wa TFF Karia alitoa hutuba fupi ambayo aliitaka kamati yake kuchapa kazi kwa bidii ili kurudisha imani ya Tanzania katika mchezo huo ambao unaongozwa kwa kuwa na mashabiki wengi nchini.

“Katika ilani yangu nina vitu ambavyo vinaonekana vidogo lakini sio hivyo kama inavyodhaniwa, nitahakikisha navisimamia kwa umakini ili kurudisha mpira wa Tanzania kwenye levo inayotakiwa,”alisema Karia.

Kiongozi huyo alisema katika uongozi wake atahitaji kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo na kwa waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini.

No comments