WATATU SERENGETI BOYS WAPATA ULAJI TUNISIA

WACHEZAJI watatu waliokuwa kwenye timu ya soka la taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Ally Ng’anzi, Yohana Oscar Nkomola na Erick Nkosi wameondoka nchini alfajiri ya juzi kwenda Tunisia kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Serengeti Boys ikiundwa na vijana wenye vipaji kutoka mikoa tofauti, iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya vijana kucheza fainali za Afrika baada ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mwezi Mei, mwaka huu nchini Gabon.

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu wa Cambiosso Sport Center, Twaha Ngwambi, vijana hao wote wamepata mwaliko wa klabu ya Etoile du Sahel ya Ligi Kuu ya Tunisia.

Ngwambia amesema mwaliko huo unafuatia vijana hao wote kufanya vizuri wakiwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka huu.

“Hii klabu ilivutiwa na hawa vijana baada ya mechi ya awali tu ya Serengeti Boys kabla ya hata ya kwenda fainali Gabon, lakini ilishindikana kwenda mapema kwa sababu ya maandalizi ya fainali za Gabon kwa sababu walikwenda kuweka kambi Morocco mwezi mzima,” alisema.

Ngwambia amesema kwamba ng’anzi na Nkosi wamekwenda kufanya majaribio, wakati Nkomola anakwenda moja kwa moja kujiunga na Academy ya timu hiyo ambako atasaini mkataba.


Pamoja na kutolewa katika hatua ya makundi nchini Gabon, Serengeti Boys ilivutia kwa soka yake, huku vijana wengi wakitabiriwa kufika mbali zaidi kisoka.

No comments