WENGER AKUBALI LAWAMA ZA ARSENAL KUMALIZA NAFASI YA TANO MSIMU ULIOPITA

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema anastahili lawama zote baada ya timu yake kumaliza nafasi ya tano msimu uliopita. Arsenal msimu ujao hawatashiriki Michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, UEFA baada miaka zaidi ya 20.

Wenger amesema kushindwa kwake kuongoza vizuri wachezaji msimu uliopita kwenye vyumba vya kubadilishia nguo lilikuwa tatizo kubwa ambalo hataki kulirudia tena msimu huu.

Hadi sasa kocha huyo amesaini wachezaji wawili tu, huku wawili wakifanikiwa kuongeza mikataba baada ya msimu uliopita kumalizika. Kushindwa kwake kuongoza vizuri kulileta mpasuko ambao uliwafanya kukosa ‘top four’ msimu uliopita.

Mashabiki wa Arsenal kwa kiasi kikubwa waliandamana msimu uliopita wakitaka kocha huyo aachie ngazi sababu timu yao imeshindwa kubeba makombe makubwa kwa miaka zaidi ya 10 sasa.


Timu hiyo ilianza vizuri mchakato wa ufunguzi wa ligi kwa kuwafunga Chelsea kwenye Ngao ya Jamii. Leo usiku wanatarajiwa kucheza na Leicester City kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England.

No comments