ABDI BANDA AZIDI KUTAKATA AFRIKA KUSINI

BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda ameonekana kuwa lulu katika kikosi chake cha Baroka FC ya nchini Afrika Kusini alikohamia akitokea Simba na sasa amekuwa akipiga dakika zote tisini akiwa mkali zaidi.

Juzi beki huyo ameisaidia klabu yake hiyo kushinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, Chippa United katika mchezo wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth.

Mabao ya Baroka yalifungwa na James Okwuosa aliyejifunga dakika ya 41 na Gift Motupa aliyefunga mawili dakika ya 63 na 89, wakati la wenyeji lilifungwa na Katlego Mashego kwa penati dakika ya 57.

Huo ni mchezo wa tatu wa Ligi Kuu ya PSL kwa Baroka na Banda msimu huu na ni ushindi wa kwanza baada ya awali kutoa sare mbili, kwanza 0-0 na Polokwane City ugenini Agosti 19 na baadae 1-1 na Orlando Pirates nyumbani Agosti 22.

Banda ndie aliyeinusuru Baroka kulala nyumbani mbele ya timu ya kocha wa zamani wa Uganda, Mserbia Milutin Sredojevic “Micho” baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 72 kwa kichwa akimalizia kona, kufuatia Thabo Qalinge kuanza kuifungia Pirates dakika ya 41.

Baroka sasa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa PSL inayoshirikisha timu 16 kwa pointi zake tano, nyuma ya Orlando Pirates, Cape Town City FC, Mamelodi Sundowns na SuperSport United zenye pointi sita kila moja.


Beki huyo amekuwa akiaminiwa na kikosi hicho kutokana na utulivu wake lakin I pia namna anavyopiga krosi zenye madhara kwa lango la adui.

No comments