AISHI MANULA APANIA KUWEKA REKODI MPYA SIMBA SC MSIMU HUU

KIPA namba moja wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, Aishi Manula amesema kwamba amepania kuandika historia mpya katika maisha yake akiwa na Simba.

Manula amesema kwamba amesajiliwa na Simba kwa ajili ya kuisaidia klabu hiyo kupata mafanikio, lakini mafanikio makubwa ambayo anayawaza ni kwamba Simba itwae taji la Ligi Kuu ya soka Tanzania bara lakini pia kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho.

“Kwa muda mrefu sasa Simba haina mataji ya Ligi Kuu na mimi nimesajiliwa hapa pamoja na wenzangu kusaidia kupatikana kwa mataji na kutokana na usajili huo mzuri tutafanikiwa,” alisema Manula.

Lakini pia kipa huyo amesema kwamba yete binafsi anataka kuendeleza rekodi yake ya kuwa kipa bora katika msimu wa tatu mfululizo wac Ligi Kuu Tanzania bara.

Kwa misimu miwili mfululizo, Manula amekuwa ndie kipa bora wa Ligi Kuu akiwa na kikosi cha Azam FC ambayo amekuwa akiitumikia kwa muda mrefu kabla ya msimu huu kuhamia kwa wekundu hao wa Msimbazi.

Pamoja na Manula, makipa wengine waliosajiliwa na Simba msimu huu ni Said Mohammed Nduda ambaye ametoka katika kikosi cha Mtibwa Sugar ya Morogoro na Emmanuel Mseja ambaye amesajiliwa akitokea kikosi cha Mbao FC ya Mwanza.


Simba wamelazimika kuachana na makipa wake, Daniel Agyei ambaye amerejea kwao Ghana pamoja Peter Manyika ambaye amesajiliwa na kikosi cha Singida United cha mkoani Singida.

No comments