AYA 15 ZA SAID MDOE: KIBA, DIAMOND, BONGO FLEVA SASA NI MWENDO WA BIG G KWA ARI MPYA NA KASI MPYA


Hivi karibuni, mchambuzi mmoja wa soka hapa nchini, Zaka Zakazi aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook maneno haya: “Ronaldo na Messi wanaziba nyota za akina Neymar. Ni sawa na Ali Kiba na Diamond. ‘Utaniua’ ya Jux ni kali zaidi ya hizo...basi tu!”

Hapo Zaka Zakazi alikuwa akimaanisha kuwa nyimbo mpya “Zilipendwa” ya Diamond na vijana wake wa WCB na ile ya “Seduce Me” ya Ali Kiba hazifikii makali ya kitu kipya cha Jux “Utaniua”. Namuunga mkono kwa asilimia 100.

“Zilipendwa” na “Seduce Me” ni nyimbo za kawaida sana, nyepesi mno, waandishi wake hawajaumiza kichwa labda tu niwapongeze kwa wazo (idea) la nyimbo, lakini hakuna nyama ndani yake, hakuna ‘melody’ zinazofanana na ukubwa wa majina ya waimbaji. Hizi ni aina ya nyimbo zinazostahili kuitwa Big G, zitaisha utamu ndani ya muda mfupi.

Ni ukweli usio na ubishi kuwa Diamond na Kiba wamelikamata soko, media zinasubiri kazi zao mithili ya mtoto mchanga anavyoliganda titi la mama yake. Chochote wanachokileta sokoni kitapokewa kwa mikono miwili kiwe kibaya au kizuri.

Kiba na Diamond kwa sasa ni watu pekee wanaoweza kuiaminisha jamii kuwa tui la nazi ni maziwa na ikakubalika bila ubishi, huu ni wakati wao na wao pia wamejua kuwa huu ni wakati wao ndio maana wala hawaumizi kichwa, wanajua chochote wakachotulisha tutakula tu.Zipo nyimbo nyingi nzuri sana za bongo fleva ambazo wasanii wake wameumiza vichwa na kuibuka na vitu adimu, lakini bado nyota zao zimezimwa kwa mfumo uleule wa Ronaldo na Messi katika soka. Tazama ujio wa Beka Flavor na Aslay halafu utanielewa.

Unapotoa nyimbo yako halafu ikakutana sokoni na ngoma ya Diamond au Kiba basi ujue hutofautiani sana mtu anayechezea shilingi kwenye tundu la choo. Ni lazima nyimbo yako igeuzwe kuwa mchezaji wa akiba.

Diamond na kundi lake la Wasafi wamekuwa wakitengeneza utitiri wa nyimbo, hatua inayofanya WCB iwe na wastani wa nyimbo mpya kila mwezi. Mfumo huu wa WCB haukuja kwa bahati mbaya, ni mkatati maalum wa kulifanya chama hilo liwe macho kwa saa 24 kuhakikisha hakuna kazi nyingine inayofurukuta sokoni- ukiweka kitu wanakuwekea kitu.

Athari ya Diamond na Kiba kutoa nyimbo za kawaida ni kubwa sana kwasababu wasanii wengi wa kizazi kipya kioo chao ni wao (Kiba na Diamond), wananakili kila mkakati wao na mwisho wa siku zitajazana nyimbo za kawaida.

Sasa tunaelekea kwenye hatua ya kuzalisha nyimbo za kawaida, nyimbo za kudumu kwa wiki nne au tano kisha zikapisha nyingine. Tangu zamani muziki wa kizazi kipya uliitwa Big G, lakini sasa tunabisha hodi kwenye mwendo wa Big G kwa ari mpya na kasi mpya.

Dunia ya bongo fleva inakwenda kasi sana katika ulipuaji wa kazi, hawaoni tena haja ya kuumiza vichwa, waumize vichwa kwa kipi wakati nyimbo zao zinachezwa kila kona? Kama video ikiingia You tube ndani ya saa 24 tayari ina watazamani 500,000 unataka nini tena?

Jamaa wana nyenzo nyingi sana, kurasa zao za mitandao ya kijamii zimejaa wafuasi lukuki, wafuasi ambao wameshakunywa maji ya bendera, wako tayari kutetea kwa nguvu zote chochote kile kinachozalizwa, neno ‘mbaya’ kwao ni msamiati mgumu sana.

Wakati msanii wa muziki wa dansi anaweza kusubiri hadi miaka mitano nyimbo yake kupata watazamani 500,000 You tube, bongo fleva inawachukua saa 24 tu, hii ni kwasababu wamejua kutumia vizuri ule usemi wa dunia ipo kwenye kiganja lakini kwa bahati mbaya sana wanatumia faida hiyo kutulisha nyimbo moja mara 10, kinachobadilika ni jina tu lakini ujumbe, mpangilio wa vyombo na uimbaji ni ule ule.

Wakati wasanii wa dansi wakiumiza vichwa kufikiria kutengeneza wimbo mpya, kwa kufanya mazoezi mwezi mzima, kubishana kwa hoja, kufuata vigezo vya uimbaji na muziki kwa ujumla, bongo fleva wao wanahitaji siku moja au mbili kukamilisha wimbo, tena wimbo ambao unaweza kutengenezwa na watu wasiozidi watatu!!.

Wakati muziki wa dansi ukiandaliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja lakini kwenye mitandao ya kijamii ukapigiwa debe kwa siku moja tu, bongo fleva wao wanatengeneza wimbo kwa siku moja lakini wanaupigia kampeni mitandaoni mwezi mzima, wanaikamata dunia na baada ya hapo kazi inayobakia kwao ni nyepesi tu, Big G kwa kwenda mbele.

No comments