AYA 15 ZA SAID MDOE: REMIX YA "UMBEYA HAUNA POSHO" YA TWANGA PEPETA NI ZAIDI YA CHENGA ZA MWILI


JUMAMOSI usiku nilipata wasaa wa kupita Mango Garden, Kinondoni kwaajili ya kuangalia onyesho la The African Stars “Twanga Pepeta”, moja ya bendi bora kabisa za dansi hapa nchini.

Naam kama nilivyosema siku kadhaa zilizopita kuwa ukumbi huo utabomelewa wakati wowote kutoka sasa hivyo unapokwenda Mango Garden kuangalia burudani, angalia kwa makini huku ukijaribu kuhisi kuwa pengine hilo ndiyo onyesha la mwisho kufanyika hapo Mango Garden.

Jumamosi mbili zijazo Twanga Pepeta watakuwa mikoani na hatujui kama baada ya hapo Mango Garden bado itakuwa ‘hai’ au la na hata Luizer Mbutu, kiongozi wa Twanga alisema kuonana ni majaaliwa na pia itatagemea hatma ya bomoa bomoa ya ukumbi huo.

Katika kuangalia na kusikiliza kwangu kwa makini burudani ya Twanga, nikavutiwa sana na utambulisho wa wimbo mpya “Umbeya Hauna Posho (Remix)”. Nikausikiliza kwa makini sana, niliusikiliza kwa sikio la uchunguzi, sikio la udadasi, sikio la kujifunza kitu fulani.

Ijumaa iliyopita, Saluti5 iliandika juu ya Twanga Pepeta kuingia studio kurekodi remix ya Umbeya Hauna Posho, marejeo ya wimbo wao wa mwaka 2001 kupitia albam yao ya “Fainali Uzeeni”. Maoni yaliyofuata baada ya hapo si mchezo, yalikuwa ni zaidi ya mashambulizi (ya nia njema lakini) kwa Twanga Pepeta.

Mengi kati ya maoni hayo, yaliashiria kufilisika kimuziki kwa Twanga Pepeta, kupoteza dira. Kwamba katika soko hili gumu la muziki wa dansi, suluhisho ni kutoa nyimbo mpya na sio kurudia nyimbo za zamani. Hii ndiyo sababu kuu iliyonifanya niusikilize kwa makini wimbo huo pale Mango Garden na baada ya kuusikiliza nikabaini kuwa kuna sehemu Twanga Pepeta wameteleza aidha kwa bahati mbaya au kwa makusudi, kuna sehemu wamejipiga wenyewe chenga za mwili.


Kwanza labda  nieleze ninavyoelewa maana ya remix katika muziki. ‘Remix’ ni kurudia wimbo mzima au sehemu kubwa ya wimbo, lakini ikiwa imeongezewa baadhi ya vitu ili kuendana na soko la wakati au sehemu husika. Inaleta maana zaidi pale  wimbo unaporudiwa katika staili tofauti ya muziki kutoka ile iliyotumika awali.

Kufanya remix si kosa na wala si kuishiwa, ili mradi tu upite kwenye misingi stahiki, uwe na sababu za msingi za kufanya hivyo, utumie wimbo ambao unaamini kuwa ulipendwa, kukubalika na kufahamika mithili ya wimbo wa taifa, wimbo ambao utashtua na kutekenya hisia za watu. Kinyume na hapo hutaeleweka – si kwa  wateja wa zamani wala wateja  wapya.

Kwa nilivyousikiliza “Umbeya Hauna Posho” (Remix), nimebaini ule ni wimbo mpya kabisa, hakuna remix pale na kwa hakika Twanga Pepeta hawakuwa na sababu ya kusema wamefanya remix, nina uhakika hata wadau waliokuwa wanasukuma mashambulizi wakibahatika kuusikiliza watakubaliana na mimi kuwa ile si remix ya “Umbeya Hakuna Posho” na watapangusa ‘povu’ zao zilizowatoka.

Katika wimbo ule kitu pekee kilichochukuliwa kwenye Umbeya Hauna Posho, ni sehemu inayosema “Pili pili ya shamba yawawashia nini… mmesutwa mnamanga manga” baada ya hapo vitu vingine vyote ni vipya kabisa. Hata neno lenyewe Umbeya Hauna Posho halipo kwenye hii remix.

Huu ni wimbo mpya wenye kionjo kutoka wimbo wa Umbeya Hauna Posho. Haustahili kuitwa remix wala ‘part two’ ya Umbeya Hauna Posho. Walichokifanya Twanga hakina tofauti na kilichofanywa na Darasa, Belle 9 au Diamond kupitia wimbo wa “Maria Salome” (Chambua Kama Karanga) wa Saida Karoli, hawakufanya remix bali walinyofoa mapigo na vionjo tu.

Kama wimbo ule umerekodiwa kwa namna ile niliyoisikia Mango Garden, basi ni bonge la wimbo kuanzia uimbaji, rap, hadi upigaji. Dosari pekee ninayoiona ni jina wimbo wimbo. Kuna maneno mazuri ambayo yangetosha kubeba jina la wimbo.

Kwangu mimi naona wimbo ungeitwa “Ziba Masikio”, “Pili Pili” au “Yawawashia Nini”, ingependeza zaidi. Maneno yote hayo yapo ndani ya wimbo na naona Twanga bado hawajachelewa kubadili jina wimbo huu ambao naamini utakuwa moja ya kazi bora za dansi kwa mwaka 2017.

Binafsi huwa sikubaliani na wimbo kupewa jina ambalo hulikuti ndani ya nyimbo, hizi mimi huwa naziita nyimbo ambazo hazijaenda ‘jando’, hii ni zaidi ya kujipiga chenga za mwili. Bendi nyingi zinafanya makosa haya, Twanga Pepeta pia walifanya kosa kama hili kwenye wimbo “Ganda la Muwa”.

Lakini mwisho wa yote nichukue fursa hii kuwapongeza Twanga Pepeta kwa ubunifu huu waliofanya wa kutumia vionjo vya nyimbo zao za zamani, nitafurahi sana kama jambo hili litakuwa endelevu kwa nyimbo zao zijazo.

No comments