AYA 15 ZA SAID MDOE: TULIKUPENDA SANA MANGO GARDEN LAKINI MWEKEZAJI AMEKUPENDA ZAIDI


Hakuna jambo linaloumiza kama kuondokewa, kupotelewa au kuvunjika kwa huduma ambayo bado hujaichoka wala kuikinai na inatesa zaidi hasa unapokosa uhakika wa mbadala wake.

Zaidi ya miaka mitatu iliyopita ukumbi maarufu wa DDC Magomeni Kondoa ulivunjwa kwa kubomolewa hadi tofali la mwisho, ikiwa sehemu ya mpango wa kujengwa jengo la kitega uchumi na kwa bahati mbaya sina uhakika kama mradi huo umeanza au la.

Lakini wakati DDC Magomeni Kondoa inavunjwa, hakukuwa na pengo lolote katika biashara ya muziki na sanaa kwa ujumla wake kwa vile kibiashara ukumbi huo ulishakuwa kimeo na hakuna bendi yoyote iliyowahi kutumbuiza pale tangu kuingia kwa mwaka 2000.

Starehe pekee iliyokuwa ikipatikana DDC Magomeni Kondoa (tena kwa msimu) ni mapambano ya ndondi - hakuna zaidi ya hicho.

Zipo kumbi nyingi za aina ya DDC Magomeni Kondoa ambazo zilikufa kibiashara (ya muziki) kama vile DDC Keko, Vijana Social Hall, New Msasani Club, Bahama Mama, Da’ West Park, Vatican City na nyingine nyingi ambazo zimeguka kuwa ‘hall’ za harusi au nyumba za ibada.

Kumbi za namna hii hazina chochote cha kuleta majonzi kwa mashabiki wa sanaa pindi zinapobomolewa kwa vile tayari zilishajitenga mapema na kazi za sanaa aidha kwa bahati mbaya au kwa makusudi.


Ukumbi wa Mango Garden Kinondoni utavunjwa muda wowote kutoka sasa ili kupisha ujenzi mkubwa wa jengo la kitega uchumi kupitia Umoja wa Vijana wa CCM na mwekezaji ambaye bado hajatajwa jina.

Hili ni pigo kwa wapenzi wa burudani kwa vile ukumbi huo bado ulikuwa bidhaa muhimu kwa sanaa ambapo maonyesho mengi ya muziki yalikuwa yakifanyika hapo kila wiki.

Kwa zaidi ya miaka 15 mfululizo, bendi maarufu ya The African Stars “Twanga Pepeta” imekuwa ikipatikana ukumbini hapo kila Jumamosi na ndiyo imekuwa ngome kuu ya kundi hilo linalomilikiwa na Asha Baraka, lakini Mango Garden pia ilikuwa ni ‘sebule’ ya wadau wa muziki ambao hata mchana hiyo ndiyo iliyokuwa sehemu yao kuu ya kukutana, kubadilishana mawazo na kupata mlo wa mchana pamoja.

Kundi la taarab la Mashauzi Classic la Isha Mashauzi limekuwa likipatikana Mango Garden kila Alhamisi kwa miaka sita mfululizo, achiliambali bendi nyingine tofauti tofauti zilizokuwa zikipokezana kuutumia ukumbi huo siku za Ijumaa.

Hii ndiyo Mango Garden tuliyoizoea, Mango iliyotupa raha tangu ilipokuwa na uzio wa michongoma, kijukwaa cha uongo na kweli na sakafu ya udongo hadi leo hii ukiwa na sura inayotazamika na mandhari ya kuvutia.

Hii ndiyo Mango Garden iliyozilea bendi za Twanga Pepeta kwa zaidi ya miaka 15, Jahazi Modern Taarab kwa zaidi ya miaka minne kabla ya kupokewa na Mashauzi Classic iliyodumu kuanzia mwaka 2011 hadi hivi sasa.

Hii ndiyo Mango Garden iliyokuwa ngome kubwa ya wapenda burudani wa Kinondoni na maeneo ya jirani ambao sasa watalazimika kusafiri hatua kadhaa kwenda kukidhi kiu yao. Twanga Pepeta na Mashauzi Classic nao hawana budi kufungasha virago mapema vinginevyo ipo siku ubomoaji utaikumba Mango sambamba na vyombo vya moja ya bendi hizo. Bomoa bomoa hainaga adabu ati!.

Taarifa za kuvunjwa kwa Mango Garden zilianza kuvuja miezi minne iliyopita ambapo ilielezwa kuwa mwezi huu wa Septemba wapangaji wanatakiwa kuondoka na kukabidhi eneo hilo kwa mmiliki (Umoja wa Vijana wa CCM) tayari kwa kubomolewa.

Ni wazi kuwa Umoja wa Vijana unaamini kuwa faida watakayopata kwa kushushwa mjengo wa uhakika ni kubwa kuliko kodi wanayolipwa na Mango Garden na huwezi kuulamu uamuzi huo, ila hiyo haituzuii kusema ‘Mango Garden tulikupenda sana, lakini mwekezaji amekupenda zaidi’.


No comments