BARNABA: SOKO LA ALBAM LIPO ILA WASANII WATENGENEZA ALBAM NDIO HAWAPO


Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya Barnaba Boy amesema si kweli kuwa albam hazina soko bali wasanii wenye uwezo wa kutengeneza albam bora ndio hawapo.

Akiongea na kipindi cha Lete Raha cha Capital Radio wiki iliyopita, Barnaba akasema wasanii wengi wanakimbilia kusema albam haziuzi wakati hata uwezo wa kutoa nyimbo moja kali kila baada ya miezi sita hawana.

“Kutengeneza albam yenye nyimbo zote kali sio jambo la mchezo mchezo, linahitaji uwezo wa hali ya juu na ndio maana wasanii wengi wanaishia kutoa ‘single’ kwa kisingizio cha kusema albam haiuzi,” alisema Barnaba.

Msanii huyo amesema yuko mbioni kutoa albam na ana uhakika itamwingizia kipato kikubwa.

Alipoulizwa juu ya ukame wa wasabambazaji wa albam, Barnaba akasema hilo kwake sio tatizo kwani ana uhakika kuna mashabiki wengi wanataka kumfikia alipo kwa njia yoyote ile.

“Nimeanza mazungumzo na makampuni na mashirika makubwa na tunaandaa mkakati mzuri utakaotumika kusambaza albam yangu nchi nzima,” alifafanua Barnaba.

No comments