CHAZ BABA AUSIFIA WIMBO MPYA WA CHOKORAA LAKINI ASEMA DAWA YAKE IKO JIKONI


Mwimbaji nyota wa dansi, Chaz Baba (pichani), amesifia kazi mpya ya Mapacha Watatu Original chini yake Khalid Chokoraa, lakini akasema anaingia ‘msituni’ kwaajili ya wimbo huo.

Akiongea katika kipindi cha ‘Weekend Bonanza’ cha Clouds FM Jumamosi usiku muda mfupi baada ya wimbo huo “Yananitesa” kutambulishwa rasmi kituoni hapo, Chaz Baba akasema huku ndiko dansi inapotakiwa kuelekea.

“Soko la sasa linahitaji nyimbo kama hizi, ni wimbo mzuri sana, lakini naamini nitaufunika muda si mrefu,” alisema mwimbaji huyo katika maongezi yake na mtangazaji Khamis Dacota.

Chaz akaongeza: “Mimi na swahiba wangu Jose Mara kupitia Mapacha Music Band, tunaandaa kazi mpya na tutahakikisha tunatoa wimbo mkali wa kuupiku huu wa Chokoraa na bendi yake.

“Tunatakiwa tupongezane pale unapoona msanii mwenzako katoa kazi nzuri halafu baada ya hapo unatafuta njia ya kutoa kilicho bora zaidi”.


No comments