CHOKORAA KUVAMIA CLUB MASAI JUMATANO OKTOBA 4 LAKINI ASITUMIE JINA LA MAPACHA


Khalid Chokoraa atavamia Meridian Hotel (Club Masai), Kinondoni Jumatano ya Oktoba 4 katika show itakayojulikana kama “Usiku wa Nyumbani ni Nyumbani”.

Kwa muda mrefu Chokoraa amekuwa ni mtoto wa nyumbani hapo Meridian Hotel tangu akiwa na bendi ya Mapacha Watatu na baadae Twanga Pepeta kabla hajaamua kuanzisha bendi yake binafsi Mapacha Watatu Original.

Inaaminika hata hatua ya Twanga Pepeta kupiga Meridian Hotel kila Jumatano, ilikuwa ni juhudi zake binafsi.

Sasa baada ya yeye kuanzisha bendi yake na huku Twanga Pepeta wakiondoka Meridian Hotel, hatimaye Chokoraa anarejea nyumbani kimtindo katika harakati zake za kutaka kuziba nafasi ya Twanga Jumatano.

Onyesho hilo la Oktoba 4 litakuwa ni la bendi mbili - Chokoraa na bendi yake pamoja na Wakali Wao Modern Taarab chini yake Thabit Abdul.

Hata hivyo kwa kuanzia, Chokoraa amepewa sharti la kutotumia jina la Mapacha Watatu kwenye onyesho hilo la kwanza.


Saluti5 imeambiwa kuwa utawala wa Meridian Hotel umesema hauwezi kuwa na bendi mbili zinazotumia jina la Mapacha kwenye ukumbi wao. Mapacha nyingine inayopiga hapo kila Jumapili ni Mapacha Music Band ya Jose Mara.

Chokoraa ametakiwa kusema "Chokoraa na bendi yake" na si kutaja Mapacha Watatu.

No comments