CRISTIANO RONALDO AFUNIKA REKODI YA PELE ...Messi bado sana


Cristiano Ronaldo ameifungia Ureno mabao matatu (hat-trick) katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Faroe Islands katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Nyota huyo wa Real Madrid mwenye umri wa miaka 32, hii inakuwa ni 'hat-trick' yake ya tano kuifungia nchi yake.

Ronaldo sasa anafikisha jumla ya mabao 78 kwa timu ya taifa na kumpiku mchawi wa soka duniani Pele aliyefikisha magoli 77 kwa Brazil.

Wakati Pele anashika nafasi ya saba kwa wafungaji wanaoongoza kwa magoli mengi duniani kwenye timu zao za taifa, Ronaldo yuko nafasi ya sita, lakini anaweza kuibuka kinara wa upachikaji wa mabao huko mbeleni kwa vile wote waliomtangulia hawachezi tena soka.

Nafasi ya kwanza inashikiliwa na Ali Daei wa Iran mwenye magoli 109, wa pili ni Ferenc Puskás wa Hungary na Spain kwa magoli yake 84 huku mpinzani mkubwa wa Ronaldo, Lionel Messi akikamata nafasi ya 27 kwa kutikisa nyavu mara 58 akiwa na nchi yake ya Argentina.


No comments