HIVI NDVYO FELLAINI ALIVYOJIBU KWA VITENDO SIFA KIBAO ALIZOPEWA NA MOURINHO

Marouane Fellaini jana alikuwa nyota wa mchezo wakati Manchester United ilipoiadhibu Basle 3-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fellaini aliyeingia dakika ya 19 kuchukua nafasi ya Paul Pogba aliyeumia, alifunga bao la kwanza na kupika goli la tatu lililowekwa wavuni na Rashford.
Kiwango bora kilichoonyeshwa na Fellaini kilikuwa ni kama majibu kwa kocha wake Jose Mourinho ambaye siku moja kabla, alimimina sifa nyingi kwa nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji.
Jose Mourinho alisema anajihisi dhaifu kiasi bila Marouane Fellaini katika kikosi chake.
Fellaini alikosa mechi ya Premier League ambayo walitoka sare ya 2-2 Jumamosi dhidi ya Stoke City kutokana na jeraha kwenye misuli ya sehemu ya chini ya mguu.
"Ni mchezaji muhimu sana kwangu, muhimu zaidi kuliko mnavyoweza kufikiria. Najihisi dhaifu bila yeye," alisema Mourinho.
Mchezaji huyo amekuwa akipendwa na pia kuchukiwa na mashabiki wa Manchester United tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2013.


No comments