JUMA PONDAMALI AMLILIA KIPA WA ZAMANI WA HARAMBEE STARS

KIPA wa zamani wa Timu ya Taifa Juma Pondamali amesikitishwa na taarifa za kifo cha kipa mwenzake kutoka Harambee Stars Mahmoud Mohammed na kusema wamepoteza mtu aliyekuwa na mchango mkubwa kwa soka la Afrika Mashariki kwa ujumla.

Mohmoud Mohammedd amefariki Jumanne kwa matatizo ya moyo akiwa na miaka 68 baada ya kurejea kutoka India alipokwenda kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kipa huyo alitumikia timu yake ya Taifa ya Harambeee Stars na klabu ya FC Leopards miaka ya 1968-74.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa, Pondamali alisema taarifa hizo amezipokea kwa masikitiko makubwa kwakuwa alikuwa karibu na marehemu kwa kipindi kirefu na pia alililetea Taifa lake heshima katika mashindano mbalilmbali.

‘’Nimesikitika sana na taarifa hizi, Mahmoud alikuwa ni tegemeo kubwa kwa Taifa lake, alisaidia katika mashindano mengi, alikuwa kipa ambaye huwezi kumfunga penati zote lazima adake hata tatu au mbili, aliweza kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania, nafikiri Kenya wamepata pigo kubwa sana,’’ alisema Pondamali.

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba Idi Pazi alisema kifo cha kipa huyo si pigo tu kwa wakenya bali kwa wanamichezo wote kwa kuwa alikuwa na mchango mkubewa katika mashindano mbali mbali ya Afrika mashariki kwa ujumla.


Kipa huyo amezikwa Jumatano jioni katika makaburi ya Allidina yaliyopo Mombasa, Kenya.

No comments