KOCHA NJOMBE MJI AJIPA MATUMAINI YA KUTUSUA LIGI KUU MSIMU HUU

LICHA ya kupoteza mechi mbili mfululizo, kocha wa Njombe Mji, Hassan Banyai amesema timu hiyo bado ina nafasi ya kufanya vizuri na kuwashangaza watu.

Banyai amesema, kiufundi timu yao imecheza vizuri zaidi ya Yanga ingawa wamepoteza mechi kwa goli 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Amesema timu yake pamoja na kupoteza mechi mbili mfululizo nyumbani, lakini walikosa bahati kwani walitengeneza nafasi nyingi na kumiliki mpira lakini walikosa umakini.

“Licha ya kufungwa, bado vijana wangu walicheza vizuri na kujitoa, jambo ambalo limenipa matumaini kama kocha mkuu nikiamini kuwa kama tutaendelea kucheza kwa hali hii basi tunaweza kubadili matokeo na kufanya vizuri huko mbele,” alisema Banyai.

Kocha huyo alisema Ligi ndio kwanza imeanza hivyo kupoteza mechi mbili sio sababu ya wao kuvuruga na kupoteza mwelekeo kwani anaamini watabadilika na kufanya vyema kama ambavyo mashabiki wao wanavyotaka.

Amesema wanayo nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kiwango walichokionyesha kwenye mechi zao mbili, hivyo amewataka mashabiki wao kuondoa hofu kwani wana timu nzuri ambayo itafanya vizuri na kusalia kwenye Ligi hiyo.

Banyai amesema wanaendelea kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo kuhakikisha wanafanya vizuri licha ya kupoteza mechi zao mbili za kwanza, zote kwenye uwanja wao wa nyumbani.

No comments