MASHABIKI WAPIGANIA "MAISHA" YA MAYANGA STARS

KOCHA wa Taifa Stars, Salum Mayanga amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya mashabiki wa soka kuibua hoja ya kulitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambalo limepata utawala mpya, kutohangaika na kazi ya kutafuta kocha mwingine.

Mayanga alitangazwa Januari 4, 2017 kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Charles Boniface Mkwasa ambaye kwa sasa ni Katibu mkuu  wa klabu ya Yanga mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi kuu Tanzania Bara.

Hadi wakati huu kocha huyo amefanikiwa kuiongoza Stars katika mechi 12, ameshinda mechi sita, sare 5 na kupoteza mechi moja, wastani ambao ni mzuri zaidi ukilinganisha na kipindi cha nyuma timu hiyo ilipokuwa ikishirikiwa na makocha wa kigeni.

Mayanga aliiongoza Stars kumaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya COSAFA  2017 iliyofanyika Afrika Kusini mwishoni mwa mwezi Juni hadi mwanzoni mwa Julai.

Lakini pia hivi karibuni Stars ilifanikiwa kuifunga Botswana mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopo kwenye kalenda za FIFA.


"Hakuna haja ya kutafuta kocha mwingine huyu anatosha kwani rekodi hizi ni nzuri, labda tujaribu kuangalia tatizo la Usimba na Uyanga,’’ ilisomeka moja kati ya maoni yaliyotumwa mtandaoni.

No comments