MBWANA SAMATTA AMMIMINIA SIFA KEVIN YONDAN

NAHODHA wa Timu ya Taifa, Mbwana Samatta amemsifu beki wa Yanga, Kevin Yondan kwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa rafiki wa Kimataifa dhidi ya Botswana.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yote yalifungwa na Simon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Nchini Morocco.

Baada ya mchezo huo, Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, amesema amefurahishwa na kiwango cha Beki Yondan ambaye amerejea kikosini baada ya takriban miaka miwili.

Samatta pia alimpongeza mfungaji wa mabao yote mawili kwenye ushindi huo, Msuva ambaye anaichezea klabu ya Difaa Hassan El Jadida ya nchini Morocco.

“Botswana walijitahidi ila ilikuwa lazima wafungwe maana hawana kikosi bora zaidi yetu. Tungeshangaa kama sisi tusingeshinda maana hatuna sababu kwa sasa,” alisema.

Kwa upande wake kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alisema amefurahishwa na wachezaji ambao amewaita kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho na akiahidi kuzidi kuwapa nafasi wengine ambao hajawahi kuwaita.


Ushindi huo wa Taifa Stars ni sifa kwa Mayanga toka akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi hicho kutoka kwa Charles Boniface Mkwasa ambaye sasa ni Katibu wa Yanga.

No comments