NEYMAR AKATAA KUPEANA MKONO NA KUBADILISHANA JEZI NA BEKI ALIYEMCHEKA


Neymar amekataa kubadilishana jezi na kupeana mkono na Anthony Ralston baada ya beki huyo kinda wa Celtic  kuonekana kumcheka mchezaji huyo ghali duniani.
Ronald alicheza soka la kibabe upande wa beki ya kulia lakini akashuhudia Celtic ikinyukwa bao tano bila majibu na Paris Saint-Germain kwenye dimba la Celtic Park katika mchezo wa Champions League Jumanne usiku.
Wakati PSG ikiwa mbele 3-0, Ralston mwenye umri wa miaka 18, akaonekana kumcheka Neymar aliyedondoka na kuzawadiwa kadi njano kwa kujiangusha makusudi.
Kabla ya hapo, Ralston naye alishalimwa kadi njano na mwamuzi wa Kitaliano Daniele Orsato  kwa kuchezea rafu na hiyo inamaanisha kuwa iwapo 'danganya toto' ya Neymar ingefanikiwa, basi Ralston angepata kadi ya pili ya njano na kutolewa nje.
Marudio ya video yakaonyesha Ralston akimcheka Neymar, lakini  beki huyo alionekana pia akimkoromea  Kylian Mbappe. 
Neymar mwenye umri wa miaka 25  akajibu kejeli zile kwa kuangalia ubao wa magoli na kisha akaonyesha ishara ya bao tatu kupitia vidole vyake.
Baada ya mchezo kukamilika, Ralston akamfuata Neymar kutaka kumpa mkono na kubadilisha naye jezi lakini supastaa huyo wa Brazil akakataa.
Ralston akasema: "Sio kitu cha maana sana. Kama hivyo ndivyo alivyotaka ni poa tu. Jambo hili haliwezi kuninyima usingizi, kila mtu ana uelewa wake, kwahiyo sijali."


'
No comments