SIMBA SC KUANZISHA BENKI YAO, KITUO CHA LUNINGA

SIMBA imeamua kuwa klabu ya kwanza hapa nchini kuendeshwa na mfumo wa wanachama wake kununua hisa, lakini pia inataka kuandika historia nyingine kubwa katika medani ya soka barani Afrika.

Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema kwamba klab hiyo pamoja na mchakato huo, imepanga kuanzisha vitega uchumi vya kutisha hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya biashara itakayojulikana kama Simba Bank pamoja na kituo cha televisheni.

Imedokezwa kwamba wakati mfumo wa mabadiliko ukiendelea kufanywa, baadhi ya matajiri wakubwa katika klabu hiyo wamependekeza kuwa hisa za klabu ambazo zitabaki baada ya kuuzwa hisa kwa wawekezaji, zianzishe benki ya biashara kwa wanachama wa Simba.

"Mkakati ambao tunakwenda nao sasa ni kwamba kuna watu wamejitokeza kuanza mchakato wa kuanzishwa kwa benki ya Simba pamoja na kituo cha matangazo ya televisheni."

"Huu ni wakati wa kufanya Simba iwe imara zaidi kiuchumi na hatutaki kusikia kwamba kuna wakati klabu inakwama,’’ amesema mdau huyo.

Imedaiwa kwamba baada ya hisa asilimia 50 kuuzwa kwa wawekezaji, wanachama wa Simba nao wanahakikisha kiasi kinachobaki cha hisa zao zinaingia kwenye mfumo  mkubwa wa kibiashara.

"Tumeanza mawasiliano na benki kuu Tanzania na wametupa maelekezo ya kufanya, lakini pia tumewasiliana na watu wa TCRA kuona namna gani tunaweza kufanya Simba Tv kuwa kituo kamili cha matangazo,’’  amesema mdau huyo.

Kwa sasa TV ni program maalum ya vipindi vya matukio mbalimbali ambavyo vimerekodiwa na kuuzwa Azam televisheni, lakini sasa Simba inataka kumiliki kabisa kituo chake cha televisheni.

Kama mfumo huo utafanikiwa Simba itakuwa klabu ya kwanza katika ukanda huu kuanzisha vitega uchumi  hivyo vikubwa ambavyo vitakuwa vinaiingizia klabu hiyo fedha za kutosha na kuifanya klabu kuwa ya uhakika na mapato yake lakini pia kuwa klabu ya kwanza kutengeneza ajira kubwa.

Kwa wengi wao, wanachama hao wa Simba wanaweza kumiliki akaunti kwenye benki hiyo na kupata mikopo ya kibiashara na kwa mara ya kwanza wataona matunda ya kuwa wanachama wa klabu hiyo kubwa hapa nchini.

Mmoja wa wawekezaji wanaotarajiwa kuingia katika mfumo huo wa hisa, Mohammed Dewji ‘’Mo’’  ameshatangaza kwamba anakusudia kuwaleta klabu ya Juventus ya Italia ambao wenyewe pamoja na wengine watasaidia kuongeza nguvu ya uwekezaji katika klabu hiyo.

Habari zinasema kwamba Juventus  wanatajia kuwasili hapa nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya mchakato huo wa kibiashara ambao pia unaweza kuingia katika mifumo ambayo Simba inakusudia kuweka.

 "Simba imeamua kuwa klabu ya kwanza katika ukanda huu pengine hata katika Afrika kuwa na vitega uchumi hivyo na hata huo uwanja wake utajengwa kwa kipindi kifupi sana tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiri,’’  amesema mtoa habari huyo.

Baadhi ya klabu matajiri kabisa barani Afrika ni pamoja na T.P Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo inatajwa utajiri wake unafikia Euro milioni 7.7, wakati Raja Casabranca ya Morocco  utajiri wake unakadiliwa kufikia Euro milioni 8.13.

E.S Setf ya Algeria inatajwa kuwa na utajiri wa ukubwa wa Euro milioni 8.6, wakati majirani zake USM Alger pia ya Algeria wenyewe wako juu kwa kuwa na utajiri wenye thamani ya Euro milioni 9.65.

Zamalek SC ya Misri ambayo imewahi kuondoshwa na Simba kwenye Ligi ya mabinwa Barani Afrika, inatajwa kuwa na utajiri unaofikia Euro milioni 10.30, lakini ikiwa imefunikwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini yenye thamani ya Euro milioni 10.35.

klabu nyingine ni pamoja na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo iko juu kwa kuwa na thamani ya Euro milioni 10.48, Clabu Afrikain ya Tunisia Euro milioni 11.80, na Esperance Sportive de Tunis pia ya Tunisia Euro milioni 12.75.


Klabu ya Ahly ya Misriinatajwa kuwa ndiyo klabu tajiri zaidi kwa kuwa na umilki wa thamani ya Euro milioni 19.25, nah ii kwa mujibu wa jarida la uchunguzi na uchambuzi la Forbes, kwa kukusaidia kujua thamani halisi ya utajiri wa vilabu hivyo, Euro ya Ulaya ni sawa na shilingi 2,672 za Tanzania kwa bei ya wiki hii, na hivyo unaona Al Alhy inautajiri wa zaidi ya shilingi Trilioni 51.

No comments