SIMBA YAIBADILISHIA GIA ANGANI AZAM FC

BAADA ya kuwapa raha wanachama na mashabiki wa klabu yao kwa ushindi dhidi ya Ruvu Shooting wa mabao 7-0, sasa Simba imeamua kuifanyia umafia timu ya Azam FC kwa kukifanyia mabadiliko makubwa kikosi chao.  

Mchezo baina ya Simba na Azam umepangwa kufanyika Septemba 6, mwaka huu ambapo awali ulitakiwa upigwe leo Septemba 2, lakini umeghairishwa kupisha maandalizi ya timu ya Taifa Stars.

Katika mazoezi ya kila siku ya kikosi cha Simba, wakuu wa benchi la ufundi linaloongozwa na Joseph Omog na Jackson Mayanja, wamekuwa wakimpa mbinu mbadala John Bocco kama hatua njema ya kutaka mnyama aibuke na ushindi.

Bocco ambaye alipata majeraha katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa uliopigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, amekuwa akifanyiwa mazoezi hayo huku akiwa katika hali nzuri ya kiuchezaji.

Kocha Mayanja ameiambia Saluti5 kuwa wanamwandaa straika huyo kucheza sambamba na Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima na Juma Luizio ili timu iondoke na ushindi na kubeba pointi tatu muhimu.


Alisema, tofauti na alivyokuwa katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting ambapo mnyama aliibuka na ushindi wa mabao 7-0, kikosi kitakachocheza dhidi ya Azam kitakuwa na mabadiliko makubwa katika safu ya ushambuliaji sambamba na ulinzi.

No comments