TANZANIA BAND FESTIVAL YAWEKA HISTORIA MPYA KWENYE MUZIKI WA DANSI


Lile tamasha la muziki wa dansi lililopewa jina la Tanzania Band Festival linarejea tena mwaka huu, lakini safari hii linakuja kivingine.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania Band Festival ilifanyika mwezi Julai mwaka jana ndani ya viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam huku zaidi ya bendi 10 zikishiriki.

Lakini safari hii, tamasha hilo linajitanua zaidi ambapo sasa litafanyika katika mikoa kadhaa tofauti na mwaka jana.

Tanzania Band Festival itaanza kurindima mjini Kahama Ijumaa Oktoba 6 katika Uwanja wa Kahama na kufuatiwa na show ya jijini Mwanza Oktoba 7 ndani ya Rock City Mall.

Bendi zitakazoshiriki maonyesho ya Mwanza na Kahama ni FM Academia, Twanga Pepeta, Msondo Ngoma, Malaika Music Band na B Band.

Hii ni mara ya kwanza kwa zaidi ya bendi nne kukutanishwa kwenye jukwaa moja mikoani, hatua ambayo imepongezwa na wadau wengi.

Saluti5 imefahamishwa kuwa Tanzania Band Festival pia itafanyika katika miji ya Dodoma, Kigoma, Sumbawanga huku onyesho kubwa na litakalokusanya bendi nyingi zaidi likitarajiwa kufanyika Dar es Salaam baadae mwaka huu.

No comments